Asante Rwanda kwa kukubali kunusuru wasaka hifadhi walio hatarini Libya- Grandi 

27 Aprili 2021

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi ambaye bado yuko ziarani kwenye ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika, amezishukuru Rwanda na Niger kwa kuwezesha utekelezaji wa mpango wa kuhamisha wasaka hifadhi wanaokumbwa na madhila nchini Libya. 

Eneo la Gashora, takribani kilometa 60 kutoka mji mkuu wa Rwanda, Kigali, mtoto mkimbizi Hadia kutoka Somalia akitabasamu.  

Hadia pamoja na mama yake mzazi aitwaye Zeinab, na baba yake Abdulbasit walikuwa kundi la kwanza la wasaka hifadhi waliohamishiwa Rwanda kutoka Libya mwaka 2019.  

Hii leo Zeinab na Abdulbasit wanaishi kwenye kituo hiki na wana mtoto wa pili aitwaye Hajira, ikimaanisha Safari kwa kisomali wakitumai mustakabali wao utakuwa mzuri. Zeinab anasema… “Tulisikia kuwa nchi hii ni salama na siyo kama Libya. Watu wengi wakiwa Libya wana hofu ya kuwekwa vizuizini na pia iwapo watakuwa huru au la.” 

Safari yao ya Rwanda ni kupitia Emergency Transit Mechanism, au mfumo wa mpito wa dharura ambao unawaweka kwenye kituo cha dharura wakisubiri suluhu ya kudumu kama vile kurejea nyumbani kwa hiari, kujumuishwa katika jamii ya Rwanda, au kurejea nchi aliyotoka au kupelekwa nchi nyingine kama hali ni salama. 

Akiwa Rwanda, Bwana Grandi amekuwa na mazungumzo na familia za wasaka hifadhi.. “Nimezungumza na familia kutoka Somalia, na wengi wao wana simulizi za kutisha kutoka Libya za kunyanyaswa, kuteswa na hata kuwekwa vizuizini muda mrefu, wamekata tamaa. Huu ni wakati ambao wanaweza kuondokana na kiwewe.” 

Kamishna Mkuu wa UNHCR akatoa shukrani.. “Kwa kweli napenda kushukuru serikali ya Rwanda, Rais Paul Kagame mwenyewe, ambaye ilikuwa wazo lake kuzindua mfumo wa ETM nchini Rwanda miaka michache iliyopita.” 

Katika kituo hiki, UNHCR inapatiwa wasaka hifadhi huduma kama vile malazi, chakula, matibabu, mafunzo ya kazi na elimu. Halikadhalika msaada wa kisaikolojia ili kuondokana na kiwewe kitokanacho na ukatili waliokumbana nao wakiwa nchini Libya. 

Mfumo wa ETM nchini Rwanda unatekelezwa kwa pamoja na UNHCR, serikali ya Rwanda na Muungano wa Afrika na unahamisha wakimbizi kutoka maeneo hatarishi nchini Libya na kuwahamishia kituo cha Gashora. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter