Ngalawa ya kandambili yaibua ubunifu miongoni mwa vijana
Ngalawa ya kandambili yaibua ubunifu miongoni mwa vijana
Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP mwaka 2017 lilizindua kampeni ya bahari safi au CleanSeas kwa lengo la kushirikisha serikali, umma, mashirika ya kiraia na sekta binafsi katika kutokomeza utupaji taka kwenye maeneo ya bahari na maziwa.
Tangu wakati huo kampeni hiyo imekuwa moja ya kampeni kubwa duniani ya kuondokana na taka za plastiki baharini ambapo hata watu binafsi wametumia ubunifu wao kuibuka na mbinu za kuondokana na taka hizo baharini.
Miongoni mwao ni watengenezaji wa ngalawa iliyotumia taka za plastiki na kandambili na kisha kusafiri kutoka Kisumu upande wa Kenya hadi Mwanza nchini Tanzania na kisha kusafirishwa hadi Dar es salaam ili kusambaza ujumbe wa kusafisha fukwe na kutotumia plastiki.
Katika fukwe za Kigamboni jijini Dar es salaam nchini Tanzania, wananchi walitumia ujio wa boti hiyo kuzoa taka ambazo zinatishia siyo tu uhai wa viumbe vya majini bali pia binadamu.
Hii ni wakati wa kampeni iliyoenda sambamba na kuwasili kwa ngalawa iliyotengenezwa kwa taka za plastiki na kandambili. Ngalawa hii ni ya pili baada ya ile iliyosafiri kutoka Lamu hadi Zanzibar. Ali Sikanda, mtengenezaji wa ngalawa hiyo anafafanua akisema “chanzo kikubwa cha uchafuzi kwenye baharí huanzia kwenye mito, na ndio maana tulienda Ziwa Viktoria kuanzia Kisumu hadi Mwanza na sasa tumekuja Dar es salaam.”
Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP limekuwa mstari wa mbele kufanikisha kampeni hii, kama anavyoeleza Clara Makenya, mwakilishi wa UNEP nchini Tanzania akisema, “ngalawa hii pamoja na kuongeza uelewa kwa watu kuhusu athari za uchafuzi, imetoa fursa pia kwa watu kuona kuwa wanaweza kutumia taka za plastiki na kujipatia kipato kwa kutengeneza vitu kama vile mapambo. Kama kule Mwanza, vijana walionesha vitu wametengeneza kutokana na taka za plastiki na kujipatia kipato.”
Lakini Ali Skanda mtengenezaji wa ngalawa ya flipflop ana ndoto zake akisema, “baada ya kurejea nyumbani Lamu, madhumuni ni kuunda chombo kikubwa kitakachoweza kupita baharí zote za dunia na tufikishe ujumbe huu dunia nzima. Haya ndio maombi na matumaini sote tunaweza kuzuia janga la uchafuzi wa baharí unaosababishwa na plastiki zisizo na maana.”