Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali na jumuiya ya kimataifa watangaza ukame Somalia   

Katika mji wa Dinsoor, Somalia waathirika wa kiangazi wakipokea mgao wa chakula  kutoka kwa WFP. (Maktaba)
Giles Clarke/Getty Images
Katika mji wa Dinsoor, Somalia waathirika wa kiangazi wakipokea mgao wa chakula kutoka kwa WFP. (Maktaba)

Serikali na jumuiya ya kimataifa watangaza ukame Somalia   

Tabianchi na mazingira

Kufuatia hali ya ukame na makadirio ya mvua, serikali ya Somalia na jumuiya ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa hali ambayo sasa imefikia hali ya ukame, imeeleza taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura,OCHA iliyotolewa hii leo mjini Mogadishu, Somalia. 

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Somalia inakabiliwa na ukame wa wastani hadi uliokithiti. Licha ya kwamba mvua za mwezi Machi na Aprili zilianza katika baadhi ya sehemu nchini, utabiri unaonesha kwamba viwango vya mvua vitakuwa chini ya wastani. Mvua kidogo zinatarajiwa mwezi Mei na Juni huku maeneo mengi yakiathirika ikiwemo Somaliland, Puntland, na maeneo ya kati na eneo la Gedo likiathirika vibaya zaidi.  

“Somalia hukabiliwa na ukame wa mara kwa mara kila miaka tano hadi sita na ukosefu wa mvua unamaanisha hali inakuwa mbaya zaidi. Wakati huu ambapo jamii inakabiliwa na hali ngumu kwa sababu ya upungufu wa maji katika maeneo mengi nchini, athari zisizotarajiwa za janga la COVID-19 na hali mbaya ya kibinadamu nchini imepelekea maisha ya wengi kuwa hatarini.” Amesema Waziri wa masuala ya kibinadamu,Khadija Diriye. 

OCHA inasema Somalia iko katika mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi na mzunguko wa majanga yanayohusiana na tabianchi unaongezeka haraka. Tangu 1990, Somalia imepata zaidi ya majanga 30 yanayohusiana na tabianchi, ikiwa ni pamoja na ukame mara 12 na mafuriko mara 19 hali ambayo ni mara tatu ya idadi ya matuko yanayohusina na tabianchi yaliyotokea kati ya mwaka 1970 na 1990. 

Aidha taarifa ya OCHA imeeleza kuwa katika mwaka huu wa 2021, hali ya ukame inatarajiwa kuongeza idadi ya watu wasio na makazi na kusababisha madhara ya muda mrefu katika maisha na uhakika wa chakula. Takribani watu milioni 3.4 wanakadiriwa kuathiriwa na hali ya ukame kufikia mwisho wa mwaka huu wa 2021, ambapo karibu watu 380,000 wanatarajiwa kufurushwa katika makazi yao. 

“Tuko karibu kabisa na janga la binadamu katikati ya hali mbaya ya kibinadamu iliyopo tayari. Gharama ya kutochukua hatua ni mbaya sana na wakati wa kuchukua hatua ni sasa. Hatua za haraka na za pamoja, pamoja na kuongeza usaidizi na ufadhili, inahitajika sasa ili kupunguza maafa kamili. " Amesema Mratibu wa masuala ya Kibinadamu, Adam Abdelmoula. 

Mpango wa usaidizi wa masuala ya kibinadamu Somalia, HRP unahitaji dola za Marekani bilioni 1.09 kusaidia watu milioni nne, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu milioni tatu walio na uhitaji mkubwa. Hadi kufikia sasa, HRP imefadhiliwa kwa asilimia 15.