Skip to main content

Tutumie ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kupata majawabu sahihi- Guterres

Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX  umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.
© UNICEF/Ahmed Salim Yeslam
Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.

Tutumie ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kupata majawabu sahihi- Guterres

Masuala ya UM

Leo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya diplomasia kwa ajili ya amani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ni kumbusho chungu ya jinsi ambavyo dunia imeunganika.

Guterres amesema ni kwa kuzingatia kumbusho hilo ndio maana kuna udharura wa haraka wa kusaka suluhu kupitia ushirikiaono wa kimataifa kwa kuchukua hatua za pamoja za kuvuka mipaka kwa maslahi ya binadamu wote, kwa kuanzia na mgao sawiwa a chanjo kwa maslahi ya watu wote.

Katibu Mkuu amesema, "umuhimu huo unakwenda zaidi ya ushirikiano kwenye janga la Corona. Unahusisha pia vitisho vinavyovuka mpaka ambavyo tunakabiliana navyo hivi sasa: Janga la tabianchi, uchafuzi wa maji na hewa, kuenea kwa silaha na uendelezaji wa teknolojia za kisasa bila makubaliano ya maadili katika matumizi."

Tunahitaji kuwa na ushirikiano wa kimataifa uliounganika zaidi, ukiwa na uratibu wa thabiti baina ya mashirika ya kikanda na kimataifa, taasisi za kifedha na ubia wa kibinafsi na umma, amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa unaohitajika ni ule jumuishi ambao unaleta pia mashirika ya kiraia, mamlaka za kimitaa na kitaifa na wengineo kwa usawa na kwa mapana.

Zaidi ya hapo amesema, "na tunahitaji ushirikiano wa kimataifa hivi sasa, ili kuibuka kutoka kwenye janga, kukabili mabadiliko ya tabianchi, kujenga jamii thabiti na salama zaidi."

Guterres ametamatisha ujumbe wake akisema leo hii "tunapoadhimisha siku ya kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa ajili ya amani, hebu na tuazimie tena ahadi yetu ya ushirikiano wa kimataifa duniani ili kupata suluhu zenye majibu kwa watu na sayari yetu."

Siku ya kimataifa ya ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kwa amani ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba A/RES/73/127 tarehe 12 mwezi Desemba mwaka 2018 na iliadhimishwa mara ya kwanza tarehe 24 mwezi Aprili mwaka 2019.

Lengo lake ni kuhifadhi na kusongesha ushirikiano baina ya mataifa ambao ndio msingi wa chata ya Umoja wa Mataifa na ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu na pia msingi wa nguzo kuu tatu za Umoja wa Mataifa ambazo ni amani na usalama, maendeleo na haki za binadamu.