Wakulima wadogo wazalisha theluthi moja ya chakula chote duniani - Utafiti wa FAO

23 Aprili 2021

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, limefanya utatifi na kubaini kuwa wakulima wadogo wadogo katika ngazi ya kaya ndio wanaozalisha theluthi moja ya chakula chote kinacholiwa duniani. 

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Roma, Italia inaonesha kuwa mashamba matano kati ya sita duniani kote yana ekari zisizozidi mbili na eneo la shamba ni chini ya asilimia 12 lakini huzalisha asilimia 35 ya chakula duniani. 

Utafiti huo umeonesha kuwa mchango wa wakulima wadogo unatofautiana kutoka nchi hadi nchi, ambapo mchango mkubwa zaidi unatoka nchini China ambako ni asilimia 80 na ni kidogo zaidi nchini Nigeria na Brazili. 

Uchambuzi huo wa takwimu unalenga kuonesha umuhimu wa data zilizooanishwa na kuboreshwa ili kuwapatia watunga sera taswira halisi ya shughuli za kilimo duniani. 

Wakifafanua zaidi kuhusu takwimu hizo, Marco Sánchez  ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa FAO na Sarah Lowder na Raffaele Bertini waandishi wenza wa ripoti hiyo wamesema “ni vyema kuepuka kutumua maneno mashamba ya familia na kilimo cha familia kama kitu kimoja, kwa sababu idadi kubwa ya mashamba ya familia ni madogo lakini baadhi yao ni makubwa na makubwa mno.” 

Mwaka 2014, ripoti ya FAO ilikokotoa kuwa mashamba 9 kati ya 10 miongoni mwa mashamba milioni 570 duniani yalikuwa ya kifamilia na yalizalisha takribani asilimia 80 ya chakula duniani.  

Hata hivyo utafiti huu mpya ukipatiwa jina “ni mashamba yapi yanalisha dunia na mashamba yake ni madogo?- unalenga kufafanua kiwango cha ukubwa wa mashamba. 

Taarifa mpya zinakadiria kuwa kuna zaidi ya mashamba milioni 608 ya kifamilia duniani kote yakiwa na eneo la ardhi ya kilimo ya kati ya asilimia 70 hadi 80 ya dunia yote na kuzalisha asilimia 80 ya chakula chote duniani. 

Utafiti huo unakwenda mbali zaidi ukikadiria kuwa asilimia 70 ya mashamba yote, yanaendeshwa katika eneo dogo tu la asilimia 7 ya ardhi yote ya kilimo ya mashamba hayo na ni chini ya ekari moja ilhali mengine ni asilimia 14 yakidhibiti asilimia 4 ya ardhi na ukubwa ni kati ya ekari moja hadi 2 huku mengine asilimia 10 ya mashamba hayo yanatumia asilimia 6 ya ardhi na ukubwa wake ni kati ya ekari 2 hadi 5. 

FAO Tanzania
Nyuso za furaha kutoka kwa wanakikundi cha Ushindi mkoani Kigoma baada ya mavuno bora kufuatia mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka FAO ambazo walitumia kwenye shamba darasa.

 

Faida za kutambua ukubwa wa shamba 

FAO inasema uchambuzi huu ni muhimu kwa mashirika ya kimataifa na watunga sera wanaolenga kutunga sera za umma na uwekezaji kusaidia kilimo cha familia, kuongeza tiba kwenye kilimo cha kaya na kuimarisha mbinu za kipato kwa wakazi wa vijijini kama ilivyoidhinishwa na muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha kaya mwaka 2019 hadi 2028. 

Halikadhalika takwimu zinasaidia kuongeza uelewa wa hali ya mashamba ya ukubwa wa kati na mkubwa ambao jukumu lao muhimu ni kufanikisha malengo ya maendeleleo endelevu, SDGS, namba 1 la kutokomeza umaskini, namba 2 la kutokomeza njaa nan amba 10 la kushughulikia ukosefu wa usawa na 12 kuwa na mifumo endelevu zaidi ya uzalishaji. 

Utafiti huo unafafanua kuwa ukubwa wa shamba mara nyingi hauna uhusiano na uzalishaji wa mazao mahsusi ukitoa mfano Mongolia ambako mashamba yasiyomilikiwa na familia lakini yamepangwa kama vitengo vya biashara na huchangia asilimia 90 ya kilimo cha ngano. 

Nchini Tanzania, kuna kiwango kidogo cha mashamba makubwa yanayomiliki asilimia 7 tu ya eneo la ardhi ya kilimo, lakini yanawajibika na uzalishaji wa asilimia 80 ya mavuno ya ngano na asilimia 63 ya mavuno ya chai. 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter