Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani watu 4,000 zaidi wakimbia Cabo Delgado, fedha za dharura zatolewa 

Mgogoro katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji umesababisha janga la kibinadamu.
© WFP/Shelley Thakral
Mgogoro katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji umesababisha janga la kibinadamu.

Takribani watu 4,000 zaidi wakimbia Cabo Delgado, fedha za dharura zatolewa 

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani watu 4,000 wamekimbia huko Palma, kaskazini mwa Msumbiji katika wiki iliyopita, wakiongeza idadi ya wakimbizi kufikia karibia 25,000 kwa mujibu wa takwimu ziliyokusanywa na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, ambalo wiki hii limechangia dola milioni 1.2, imeeleza taarifa ya shirika hilo iliyotolew mjini Pemba nchini Msumbiji.

Mkuu wa kazi wa IOM nchini Msumbiji Laura Tomm-Bonde amesema, "mamia ya watu wenye mahitaji ya dharura ya kibinadamu wanawasili kila siku kwa miguu, basi na mashua kwa sababu ya ukosefu wa utulivu huko Palma. Tunaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha lakini tunahitaji msaada zaidi kusaidia kukuza suluhisho la kudumu kwa maelfu ya familia zilizofurushwa ili waweze kuanza kujenga mustakabali mpya wao na familia zao. " 

Shughuli za misaada ya kibinadamu za IOM kaskazini mwa Msumbiji zinafadhiliwa na mashirika ya wafadhili, kwa msaada wa mchango wa dola milioni 1.2 kutoka kwa Mfumo wa Ufadhili wa Dharura wa Uhamiaji wa IOM. Mkurugenzi wa Operesheni na Dharura wa IOM atawasili Msumbiji kesho kutathmini zaidi hali hiyo na kuthibitisha kujitolea kwa IOM kusaidia watu wenye uhitaji katika eneo hili. 

Taarifa hiyo ya IOM inasema zaidi ya nusu ya waliokimbia makazi yao wako katika wilaya za Mueda (6,970) na Nangade (6,733) kwenye mpaka wa kaskazini na Tanzania. Wengine wamehamia kusini zaidi katika mkoa wa Cabo Delgado; Watu 5,000 wamewasili katika Jiji la Pemba, na wengine 3,795 katika wilaya ya Montepuez. 

Malitate Ali, mama wa watoto sita akiwemo pia mtoto mchanga, amepata makazi katika nyumba ya mmoja wa jamaa zake Pemba na anapokea msaada wa kisaikolojia kutoka IOM, anasema,"katika Palma, vikundi vyenye silaha vilikuja, waliteketeza maduka, nyumba na kuchinja watu. Baadhi ya watu wa familia yangu walichukuliwa na kujeruhiwa. Ninahitaji chakula na mavazi kwa watoto wangu, hasa mtoto wangu mchanga. Amani ikirudi Palma, ndipo nitarudi.” 

IOM inaendelea kutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa mamia ya watu waliofurushwa kutoka Palma, pamoja na huduma ya kwanza ya kisaikolojia, ushauri kwa njia ya kundi, na usaidizi wa kibinafsi. 

Shirika hilo linasafirisha vitu visivyo vya chakula, NFIs, kuongeza shughuli za kusaidia pamoja na kuyafikia maeneo magumu. Wiki iliyopita , vifaa vilitolewa kwa takribani familia 2,000 zilizofurushwa katika wilaya za Mueda na Montepuez, pamoja na maturubai, blanketi, mavazi, ndoo, madumu na vitu vingine muhimu. 

Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2021, IOM imetoa msaada wa moja kwa moja kwa zaidi ya watu 40,000 walioathiriwa na ukosefu wa usalama huko Cabo Delgado.