Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu awajibike kurejesha hadhi ya sayari dunia:Guterres 

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.
NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Kila mtu awajibike kurejesha hadhi ya sayari dunia:Guterres 

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya sayari mama dunia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kujitolea kurejesha sayari dunia katika hadhi yake, na kufanya kila mtu kuishi kwa amani na maumbile au mazingira.  

Wito huo umo katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya mama duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Aprili. 

Guterres amesema maadhimisho yam waka huu yanafanyika wakati sayari iko katika hali mbaya, wakati binadamu wa dunia hii wanaendelea kunyanyasa ulimwengu wa asili. 

Malizeni vita dhidi ya maliasili 

Katibu Mkuu amesema "Sisi hupuuza rasilimali za dunia, tunaangamiza wanyamapori wake na tunachafua hewa, ardhi na bahari kama kuufanya kama uwanja wa kutupa taka. Mifumo muhimu ya ikolojia na minyororo ya uzalishaji wa chakula imesukumwa ukingoni na karibu inaporomoka. Hii ni kujiua. Lazima tumalize vita vyetu dhidi ya maumbile na kuyarejesha katika afya tena.” 

Bwana Guterres ameongheza kuwa kumaliza vita hivi kunataka "hatua Madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. kupunguza kiwango cha joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 Celsius. Hatua kali za kulinda bioanuwai, na kupunguza uchafuzi wa mazingira na taka, zinahitajika pia.” 

Katibu Mkuu ametoa hakikisho kwamba hatua hizi sio tu zitalinda sayari dunia ambayo ndiyo, "nyumba yetu pekee", lakini pia zitatengeneza mamilioni ya ajira mpya. 

"Kujikwamua kutoka kwa janga la COVID-19 ni fursa ya kuweka ulimwengu kwenye njia safi, inayojali mazingira, na endelevu zaidi", amesisitiza Katibu Mkuu. 

"Katika siku ya kimataifa ya Mama Dunia, wacha tujitolee kwa bidii kuirudisha sayari yetu na kuhakikisha tuna amani na maumbile". 

Wito wa kuchukua hatua 

Kwa shirika la mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, siku hii ya kimataifa ni ya kudhihirisha haja ya kuhamia kwenye uchumi endelevu zaidi ambao unanufaisha watu na sayari. 

Shirika hilo linasema, "Sayari dunia inahimiza wazi wito wa kuchukua hatua. Mali asili inateseka. Moto wa nyika Australia, rekodi za joto la kupindukia na uvamizi mbaya zaidi wa nzige nchini Kenya. Sasa tunakabiliwa na janga la COVID-19, ambayo ni kiungo cha janga la afya duniani kwa afya ya mfumo wetu ikolojia ”. 

UNEP imeandaa dokezo la utekelezaji wa Hatua za mabadiliko ya tabianchi, ambalo linatoa takwimu zinazoonyesha maendeleo ya ulimwengu katika kufikia malengo ya mkataba wa Paris wa 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi, uliosainiwa na zaidi ya nchi 190. 

"Kadiri hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi inavyozidi kuongezeka, mpito kuelekea utulivu wa hali ya hewa unazidi kuwa muhimu. Maendeleo yatategemea nchi na uwezo wao wa kukutekeleza ahadi zao chini ya Mkataba wa Paris na mwishowe michango yao ya pamoja ya kuhakikisha wastani wa joto duniani unasalia chini ya nyuzi joto 2 ° C. "