Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu kuhusu Alaa, mkimbizi ambaye ni mfano wa nguvu katika hali ya changamoto za maisha

Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
World Bank/Miso Lisanin
Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Fahamu kuhusu Alaa, mkimbizi ambaye ni mfano wa nguvu katika hali ya changamoto za maisha

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutana na Alaa, mkimbizi kutoka Syria ambaye amemudu kuwahamasisha wanawake wenzake kutoka Syria na wenyeji wake Lebanon kutumia michezo na mazoezi ya mwili ili kujenga  kujiamini na pia kujenga  jamii hata wakati wa janga la COVID-19.

Katika mji wa Anjaru ulioko kwenye bonde la Bekaa nchini Lebanon, mke na mume na mtoto wao wanafanya mazoezi ya mchezo wa ngumi na mateke au kickboxing. Sakafuni kuna vifaa vya mchezo huo na ukutani pamesheheni medali kadha wa kadha, ushahidi kwamba Alaa si wa mchezomchezo katika mchezo huu unaohitaji kurusha ngumi na mateke. Alaa anaeleza historia yake fupi ya michezo, “Tangu nilipokuwa mdogo, nilipenda michezo na aina mbalimbali za mazoezi. Nilipenda aina hii ya mazoezi kwa sababu nilihisi inaweza kunipa nguvu na nilihisi kujiamini kwangu kulikua kupitia mchezo wa ndondi za mateke.” 

Tangu akimbie Syria mnamo mwaka 2015, Alaa amewashirikisha wanawake wenzake wa Syria na Lebanon, mapenzi yake ya mazoezi.   

Kuibuka kwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kulivuruga kiasi mipango ya Alaa na wenzake, lakini wakaja na mbinu mpya kama Alaa mwenyewe anavyoeleza, “Nilipokuja Lebanon, mimi na marafiki zangu tuliishia kuwa na vipindi vya mazoezi ya mwili wakati wa mikusanyiko yetu. Kwa sababu ya COVID-19, ikawa vigumu kwetu kukutana kwa hivyo tuliamua kuendelea na vikao vyetu kwa njia ya mtandao. " 

Madarasa ya mtandaoni yanayofanywa na Alaa yamesaidia wanawake wanaopitia janga la COVID-19 kujenga nguvu, kujiamini na pia kujenga jamii hata katika maisha ya umbali wa kijamii. Mmoja wa wanufaika ni Duaa, naye mkimbizi kutoka Syria ambaye anasema, "nimekuwa nikifanya mazoezi kwa karibu mwaka. Nilikuwa na msongo wa mawazo, lakini nashukuru, uliisha katika miezi 6 ya mazoezi. Kwa kutumia mazoezi na kutembea, nilipunguza uzito, ambayo ilinitia moyo. Pia nilikutana na watu wapya kwa sababu sijui mtu yeyote katika Lebanoni, na sina familia hapa. "