Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya COVID-19 imeniondoa hofu ya kuhudumia wazazi- Mkunga Uganda

Mkunga Susan Masabe wa kituo cha afya cha Busamizi wilaya ya Buvuma kwenye visiwa vya Buvuma nchini Uganda akimpatia chanjo ya pili dhidi ya Pepopunda mjamzito Amoding Irene.
UNICEF/Henry Bongyereirwe
Mkunga Susan Masabe wa kituo cha afya cha Busamizi wilaya ya Buvuma kwenye visiwa vya Buvuma nchini Uganda akimpatia chanjo ya pili dhidi ya Pepopunda mjamzito Amoding Irene.

Chanjo dhidi ya COVID-19 imeniondoa hofu ya kuhudumia wazazi- Mkunga Uganda

Afya

Uganda, utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa wahudumu wa afya kumerejesha imani kwa wahudumu hao ambao awali walikuwa na hofu ya kwamba wanaweza siyo tu kuambukizwa wao Corona bali pia kuambukiza wagonjwa wanaowahudumia.

Ni Susan Masabe, mkunga katika kituo cha afya cha Busamuzi kilichoko kwenye kisiwa cha Buvuma ziwani Viktoria nchini Uganda, akiwa ananyonyesha mtoto wake mchanga.  

Susan anakumbuka mwaka jana mwezi Machi wakati akiwa na ujauzito wa miezi minne na ugonjwa wa Corona ukiwa ndio umeshamiri. 

Anasema kwa kuwa ilielezwa kuwa wanawake wajawazito, wanaonyonyesha na wazee wako hatarini kuambukizwa Corona, alikuwa na hofu kubwa. 

Hasa kama mkunga, kumhudumia mwanamke anayejifungua unamwambia vaa barakoa! Naye anakujibu, ninashindwa kupumua kwa kukosa oksijeni, lakini unaendelea kusisitiza, Barakoa! Barakoa! Kwa hiyo tulipata wakati mgumu sana!” 

Baada ya kujifungua salama amesharejea kazini akikumbuka mtazamo hasi waliokuwa nao wakati wanafanya kazi akisema,“Ni wafanyakazi ambao kwa sababu tuko mstari wa mbele tunapaswa kufa kwa kuwa tunaokoa wengine?” 

Tarehe 5 Machi mwaka huu chanjo dhidi ya Corona ziliwasili Uganda na siku 5 baadaye chanjo zilianza kutolewa nchini kote ikiwemo Buvuma, kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF

Buvuma ina visiwa vidogo vidogo 52 ambavyo vyote hufikiwa kwa boti ndogo ndogo na hivyo Susan alitumia fursa ya ujio wa chanjo ili naye apate chanjo. “Hakuna njia yoyote ambayo nitashawishi watu wengine wapate chanjo kama mimi mwenyewe nina mtazamo hasi. Lakini tunataka janga hili liishe. Kwa hiyo nakuwa mfano ili wengine washawishike na wapate chanjo.” 

Sasa Susan baada ya kupata chanjo hofu yote imetoweka ana matumaini yake ni kwamba chanjo sambamba na kanuni za kinga kama barakoa na usafi wa mikono vitamwezesha kuwa karibu na wagonjwa wake.