Guterres asikitishwa na kifo cha Rais Idriss Déby wa Chad

20 Aprili 2021

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake makubwa kufuatia taarifa za kifo cha Rais Idriss Déby wa Chad.

Rais Déby Itno amefariki dunia leo asubuhi ambapo Katibu Mkuu kupitia taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani leo na msemaji wake, ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake, wananchi na serikali ya Chad.

Kwa mujibu wa duru za Habari, Rais huyo wa Chad amekubwa na umauti baada ya kujeruhiwa kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo N’Djamena ambako alikuwa ameungana na jeshi la nchi hiyo kukabili waasi waliokuwa wanajaribu kupindua serikali.

Idriss Déby alikuwa mdau muhimu

Katibu Mkuu Guterres katika taarifa yake amesema Rais Déby alikuwa mdau mkuu wa Umoja wa Mataifa na amekuwa na mchango mkubwa katika utulivu kwenye eneo ka ukanda wa Sahel hususan katika kukabiliana na ugaidi, misimamo mikali na uhalifu uliopangwa kwenye ukanda huo.

Amesema "katika nyakati hizi ngumu, Umoja wa Mataifa unasimama kwa mshikamano na wananchi wa Chad katika juhudi zao za kujenga amani na mustakabali wenye ustawi."

Rais Déby ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu ambapo kifo chake kimeokea siku moja baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ya uchaguzi uliofanyika tarehe 11 mwezi huu wa Apili, ambayo yalionesha kuwa ataibuka mshindi na hivyo kuendelea kuongoza kwa awamu ya sita.

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Matiafa Volkan Bozkir ameelezea rambirambi zake kwa wananchi wa Chad.

Msemaji wa Bwana Bozkir amemnukuu akisema, "Rais wa Baraza Kuu amesema punde ataitisha mkutano wa Baraza Kuu ili kumuenzi na kumkumbuka mwendazake Deby."

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter