Waliofurushwa ndani ya Msumbiji wanasaidiana, lakini msaada wa haraka utahitajika wakiongezeka-UNHCR 

20 Aprili 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema familia zilizotenganishwa walipokimbia vurugu kaskazini mwa Msumbiji wanasaidiana wao kwa wao, lakini kadri idadi inavyoongezeka msaada wa haraka unahitajika. 

Katika eneo la Pemba kwenye kituo cha kupokea waliofurushwa ndani ya maeneo mengine nchini Msumbuji wanaonekana watu wapya waliowasili baada ya kufurushwa. UNHCR imesema idadi ya watu waliofurushwa kutokana na mashambulio ya hivi karibuni kaskazini mwa Msumbiji inaendelea kuongezeka wakati watu bado wanatafuta usalama. Tangu Machi 24 mwaka huu, zaidi ya watu 19,000 wamekimbia Palma kwenda miji ya Nangade, Mueda, Montepuez na Pemba. Maelfu zaidi wanadhaniwa kufurushwa ndani ya wilaya ya Palma. Karibu watu 700,000, hasa wanawake, watoto na wazee wamefurushwa kaskazini mwa Msumbiji, ikiwa ni matokeo ya mashambulio ya mara kwa mara na vurugu za vikundi visivyo vya serikali tangu Oktoba 2017. 

Shirika hilo la kuhudumia wakimbizi, limeonya kwamba idadi hii inaweza kuvuka watu milioni moja ifikapo Juni mwaka huu ikiwa vurugu zinazoendelea hazitakoma. Vilevile UNHCR inasema ilikuwa inaandaa hatua za kupokea watu wapya zaidi katika siku zijazo na wafanyakazi wake wanafika katika maeneo nje ya Pemba kusaidia watu wapya waliofurushwa. Abdalla Mussa, ni afisa ulinzi wa UNHCR anasema, "Tumeona familia kadhaa zikifika Pemba zikiwa na kiwewe sana na katika hali ngumu. Watu hawa kwa namna fulani wanatengwa na jamaa zao ikiwa ni pamoja na watoto waliotengwa na wazazi wao. Tunashughulikia hili pamoja na mashirika mengine ya kibinadamu na serikali kupata suluhisho kwa ajili yao. " 

Taarifa ya UNHCR inaeleza kuwa wengi wa wanaowasili ni wanawake na watoto wakiwa na mali zao kidogo, wengi wakionesha dalili za majeraha makubwa kufuatia ukatili walioshuhudia na kuwa na wasiwasi kuhusu ndugu walioachwa nyuma. Hali ya ghafla na mbaya ya shambulio hilo iliziacha familia zikigawanyika, wengi bado hawawezi kuondoka. Miongoni mwa makundi dhaifu yaliyowasili Pemba kulikuwa na watoto ambao hawajaambatana na yeoyte, familia zilizotengwa na wazee. 

Mmoja wa waliofurushwa ni Maria mwenye umri wa miaka 31, mama wa watoto watatu aliyetenganishwa na mumewe na ambaye amelazimika kukimbia nyumbani kwake mara mbili. Mnamo Machi 2020 alikimbilia mji wa pwani wa Palma baada ya vikundi visivyo vya serikali kushambulia kijiji chake huko Mocimboa da Praia kaskazini mwa Msumbiji. Sasa, mwaka mmoja baadaye, amelazimika kukimbia tena, akiacha kila kitu nyuma, baada ya Palma kushambuliwa. Maria anasema, “Moyo wangu unaniambia nisiende popote na nimsubiri mume wangu. Wakati mume wangu atakapofika hapa, tutajua wapi pa kwenda.” 

Katika kituo cha muda kilichoanzishwa na Serikali, Maria anasubiri, akitumaini atawapata watu wake na kuwa yuko salama. Yeye anautumia wakati wake kusaidia wengine. 

Maria anajitolea kwa UNHCR kuandaa majadiliano na watu wapya wanaowasili na anaeleza wanawake wengine umuhimu wa hatua za kuzuia Covid-19 na kipindupindu. Yeye pia anasaidia kutambua waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia na kuwapeleka kwa UNHCR ili wapate msaada. Maria anaeleza akisema, “Tunakaa kituoni na watu wengi na tunafanya kazi katika vikundi tofauti katika maeneo ya usafi, mawasiliano na afya. Maji pia yanatolewa kwa ajili ya kunawa mikono ili kuzuia watoto kuugua.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter