COVID-19 yakatili maisha ya watu milioni 3, kwa kushikamana tutalishinda janga hili: Guterres 

Vijana wanaojitolea nchini Jordan katika jamii zao wakati huu wa janga la COVID-19
© UNICEF/Naua
Vijana wanaojitolea nchini Jordan katika jamii zao wakati huu wa janga la COVID-19

COVID-19 yakatili maisha ya watu milioni 3, kwa kushikamana tutalishinda janga hili: Guterres 

Afya

Idadi ya vifo milioni 3 vilivyosababishwa na janga la virusi vya corona au COVID-19 imefikiwa leo Jumamosi, n ani hatua mbaya sana kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye ameomba mshikamano ili kulishinda janga hili la COVID-19

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Antonio Guterres amesema "Dunia yetu imefikia hatua mbaya , watu milioni 3 wamepoteza maisha kutokana na # COVID19. Katika kumbukumbu zao, lazima tuendelee kusonga mbele ili kila mtu, kila mahali, apate chanjo na matibabu anayohitaji haraka. #Kwa pamojaPekee, kwa kusimama pamoja, tutalishinda janga hilo,”.

Zaidi ya vifo milioni 3 vilivyosababishwa na COVID-19 vimerekodiwa rasmi duniani kote tangu kupatikana kwa virusi hivyo vipta vya corona nchini China mnamo Desemba 2019.

Wataalam wengi wanaamini kwamba , hata hivyo takwimu zawaathirika wa janga zinazotajwa ni za makadirio ya chini ukilinganisha na hali halisi , kwa sababu ya ukosefu wa uwazi kwa baadhi ya nchi na ugumu wa baadhi yanchi nyingine katika kutoa takwimu za kuaminika.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, lilisema Ijumaa kuwa idadi yawagonjwa wapya wa COVID-19 inayorekodiwa kila wiki ulimwenguni kote imeongezeka mara mbili katika miezi miwili iliyopita.

Ongezeko la kutisha la wagonjwa

Duniani kote, idadi ya wagonjwa na vifo vinavyuohusiana na COVID-19 inaendelea kuongezeka "kwa kiwango cha kutisha," limeonya shirika la WHO.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswisi jana Ijumaa alisema "Duniani kote, ujumbe wetu kwa wote, katika nchi zote, unabaki vile vile kwamba, sisi sote tuna jukumu la kuchukua hatua kumaliza ugonjwa huo”.

Katika mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC) jana Ijumaa, mkuu wa WHO pia alisisitiza kuwa usawa katika chanjo ndio "changamoto ya wakati wetu na tunashindwa kuikabili".

Alisema kati ya dozi milioni 832 za chanjo ambazo zimeshatolewa hadi sasa, asilimia 82% ilikwenda kwa nchi zenye kipato cha juu au cha kati, wakati ni  asilimia 0.2% tu zilikwenda kwa nchi zenye kipato cha chini. 

Katika nchi zenye kipato cha juu pekee, mtu mmoja kati ya wanne amepokea chanjo, uwiano ambao unashuka hadi mtu 1 kati ya 500 katika nchi masikini.