Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sababu ya COVID-19 Ramadan mwaka huu itakuwa ngumu sana kwangu: Mkimbizi Anna 

Wakimbizi katika kambi ya Mbera ambapo watoto wanahudhuria masomo.
UNICEF/Agron Dragaj
Wakimbizi katika kambi ya Mbera ambapo watoto wanahudhuria masomo.

Sababu ya COVID-19 Ramadan mwaka huu itakuwa ngumu sana kwangu: Mkimbizi Anna 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati Waislam kote duniani wakiwa wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kutana na mkimbizi Anna anayeishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Mbera nchini Mauritania, anasema anashukuru mwezi mtukufu umeanza salama, lakini utakuwa mgumu sana kwake na familia yake kutokana na janga la corona au COVID-19.

Anna akiwa kambini Mbera anasema siku za nyuma kulikuwa na watu wakarimu ambao walikuwa kila mahali na wakiwaletea nyama, tende na hata maziwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, lakini sasa  mambo yamebadilika 

“Tangu kuwasili kwa gonjwa la COVID-19 watu kama hao wameadimika kabisaa na hatuwaoni.” 

Anna na familia yake walipolazimika kufungasha virago na kukimbia alipoteza kila kitu alichokijua na kuwa nacho na sasa anaishi kambini hapa Mbera akiwahudumia na kuwalisha jumla ya watoto 9,  sita aliowazaa  mwenyewe na wengine watatu anaowalea.  

Kutokana na familia yake na pia janga la corona anasema mfungo wa mwaka huu ulioanza jana ni mtihani mkubwa kwake

“Nina familia kubwa na mwaka baada ya mwaka msaada unapungua. Ramadhan ni wakati mgumu kwetu na vitu vya msingi tunavyohitaji ni nyama na tende. Wakati unapogunga ni vuzuri kufungua swaumu kwa tende kama zipo.” 

Kila mwaka wakati wa Ramadhani shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linatoa wito wa msaada ili kuendelea kuwasaidia wakimbizi kama Anna na familia yake kwa malazi, chakula, maji na huduma za afya , lakini pia kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kidini kwa kufunga bila adha.