Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatiwa wasiwasi mkubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Uganda:UN 

Maandamano ya wanawake huko Buliisa nchini Uganda wakati wa siku ya wanawake duniani 2021.
UN/ John Kibego
Maandamano ya wanawake huko Buliisa nchini Uganda wakati wa siku ya wanawake duniani 2021.

Tunatiwa wasiwasi mkubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu Uganda:UN 

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameiomba serikali ya Uganda isitishe mara moja ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa ambao ulianza kabla ya uchaguzi mkuu wa Januari ulioleta mzozo na unaendelea kuwakandamiza wafuasi wa upinzani. 

Wataalam hao wamesema, "tumehofishwa haswa na ripoti za ukandamizaji ulioenea na unaoendelea dhidi ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Zaidi ya watu 50 wameuawa kutokana njia za kikatili zinazotumiwa na polisi, pamoja na matumizi ya risasi za moto zilizofyatuliwa bila tahadhari, na watu wengine wasiopungua 20 wamepoteza maisha katika visa vinavyohusiana na muktadha wa uchaguzi." 

Wataalam hao wmehimiza viongozi wachunguze mara moja na kwa kina matukio hayo na kushtaki ukiukaji wowote wa haki za binadamu, ikiwemo madai ya mauaji ya kiholela, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela, watu kutoweshwa kwa nguvu, kuteswa na kutendewa vibaya, kunyimwa haki ya mchakato unaofaa wa kisheria na kushambulia uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani . 

Maelfu ya watu watiwa mbaroni 

Watu elfu kadhaa wamekamatwa na wakati wengine wameachiliwa, wengine wanadaiwa kuteswa kabla ya kufikishwa katikamahakama za kijeshi, wataalam  hao wa haki za binadamu wamesema.  

Na wameongeza kuwa jamaa za wengine mara nyingi hawajui hatima yao au wapi waliko. "Inasikitisha kwamba wale ambao wanauliza habari juu ya jamaa zao waliopotea au kutoweshwa kwa nguvu wanakabiliwa zaidi na adhabu na kukamatwa. Tunaisisitiza serikali ya Uganda ichukue hatua zote zinazohitajika ili isitisha mara moja kuficha habari juu ya watu waliokamatwa katika muktadha wa uchaguzi mkuu, kitendo ambacho ni kinapelekea watu kutoweshwa, na kutanabaisha wazi hatma yao na mahali walipo. 

Wataalam hao huru wamesema “Kukamatwa kiholela na kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani kati ya tarehe 14 na 25 Januari 2021 kwa  kiongozi mashuhuri wa upinzani anayejulikana kama Bobi Wine (Bwana Kyagulanyi), ambapo mahakama Kuu iliamua kuwa ni kinyume cha katiba, ni dalili ya mbinu kali za kukandamiza za upinzani na kutokuwepo kwa haki katika mchakato wa sheria. 

Viongozi wa upinzani na wafuasi wao wameandamana kupinga madai ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na kupingwa marufuku ya mikusanyiko kwa kisingizio cha kuzuia kuenea kwa virusi vya COVID-19.  

Upelekaji mkubwa wa vikosi vya jeshi katika miji, na vile vile vitisho na mashambulio kwa waangalizi wa upinzani kwenye vituo vya kupigia kura, viliripotiwa kuathiri idadi ya wapiga kura, wakati usumbufu wa huduma za mtandao uziipunguza mchakato wa kupiga kura na kuathiri zoezi la kuhesabu. 

"Kugandamizwa kwa uhuru wa vyombo vya habari, vitisho, unyanyasaji na mashambulio dhidi ya waandishi wanaoripoti taarifa za uchaguzi na haswa upinzani haikubaliki. Serikali lazima itoe suluhisho na fidia ya haraka kwa waathirika wote," wamesisitiza wataalam hao.