Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF Sudan Kusini yamletea nuru Adut aliyekuwa hoi taaban 

Ajaba Ombacha, kutoka SUdan Kusini  mwenye umri wa miezi 17 akipimwa iwapo ana utapiamlo uliokithiri.
© UNICEF/UNI375881/Ryeng
Ajaba Ombacha, kutoka SUdan Kusini mwenye umri wa miezi 17 akipimwa iwapo ana utapiamlo uliokithiri.

UNICEF Sudan Kusini yamletea nuru Adut aliyekuwa hoi taaban 

Afya

Utapiamlo uliokithiri au unyafuzi ni tishio kubwa la uhai kwa watoto nchini Sudan Kusini ambako shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kutambua hilo linachukua hatua na sasa mtoto Adut ambaye mwaka 2019 alikuwa hoi bin taaban sasa anatembea na baba yake anajivunia.

Sauti ya baba mzazi wa mtoto Adut nchini Sudan Kusini akikumbuka mwezi Agosti mwaka 2019 akisema binti yangu Adut alikuwa ni mgonjwa mno, na nikahofua atakufa, alikonda mno kwa sababu ya utapiamlo,  

Adut alikuwa hawezi kutembea hadi ashikwe mkono. Alilazwa katika kituo cha afya cha Aweil, kaskazini-magharibi mwa Sudan Kusini kwa kipindi cha wiki nane. 

Baada ya huduma za matibabu ikiwemo na lishe bora, Adut alitoka hospitali na kurejea nyumbani ambako kupitia mradi wa UNICEF wa mgao wa lishe bora na virutubisho kwa watoto, ameendelea kukua, akiwa ni miongoni mwa asilimia 95 ya watoto Sudan Kusini wanaopona baada ya kupatiwa tiba dhidi ya utapiamlo. 

Judy Juru Michael ni afisa lishe wa Unicef Sudan Kusini na amemtembelea Adut kufahamu maendeleo yake ambapo anacheza naye kwa furaha kubwa. 

“Nina furaha sana kumuona Adut anafuraha na anacheza. Utapiamlo siyo hukumu ya kifo, unaweza kutibiwa na unazuilika.” 

Sasa Adut anakula milo mitatu kwa siku na ana uzito sawa na umri wake, na baba yake akiwa na tabasamu anafunguka akisema, “amepona, amekuwa na afya, amekuwa binti mzuri, ndio maana nina furaha na ninamshukuru Mungu kwa hilo kwamba sasa hivi binti yangu ana afya njema.” 

Nchini Sudan Kusini mwaka huu pekee watoto milioni 1.4 wako hatarini kukumbwa na Utapiamlo uliokithiri, lakini kwa msaada, ugonjwa huo unaweza kutibiwa na pia kuzuilika.