Covid-19 imeongeza ugumu katika mapambano dhidi ya Chagas inayoua takribani watu 10,000 kila mwaka

Ikiwa kesho Aprili 14 ni siku ya ugonjwa wa Chagas, shirika la kimataifa la kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani, Unitaid linaloratibiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, limesema uwepo wa Covid-19 umefanya hali kuwa mbaya zaidi kwa hali ambayo tayari ilikuwa mbaya kutokana na ugonjwa wa Chagas.
Ukiwa unaambukizwa na mdudu ambaye ananyonya damu anayeitwa Trypanosoma cruzi au T. cruzi, ugonjwa wa Chagas, kwa sasa unaathiri watu kati ya milioni 6 na 7 ulimwenguni na unaua watu wanaokadiriwa kuwa 10,000 kila mwaka, inasema Unitaid.
Aidha, Unitaid wanaeleza kuwa katika Amerika ya Kusini ambako umeenea kwa wingi, Chagas unasababisha vifo vingi kuliko ugonjwa wowote wa vimelea ikiwemo malaria. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, takriban watu milioni 75 wako katika hatari ya kuambukizwa, wengi wao wakiwa miongoni mwa watu maskini na wanaoishi pembezoni zaidi.
Licha ya viwango vya juu vya ugonjwa na mzigo mkubwa wa kiuchumi, ni asilimia 7 tu ya watu walio na ugonjwa wa Chagas wanaogunduliwa, na ni asilimia 1 tu wanaopata huduma inayofaa. Ugonjwa huu ukiachwa bila kutibiwa unaweza kusababisha matatizo makubwa ya moyo na mmeng'enyo wa chakula, linaendelea kueleza shirika hilo linaloratibiwa na WHO.
Covid-19 imeyafanya mambo kuwa mabaya zaidi. Wengi wa wale wanaougua ugonjwa wa Chagas ni miongoni mwa makundi ya watu walio katika hatari zaidi ya janga la Covid-19. Wagonjwa walioambukizwa na ugonjwa pia wako katika hatari ya kupata COVID-19 iliyo kali. Zaidi pia, kuelekeza kwa rasilimali za kupambana na magonjwa mengine, kwenda katika mapambano dhidi ya Covid-19 kumeongeza shinikizo maradufu kwenye vituo vya afya na pia wasiwasi wa wagonjwa kuoata maambukizi ya Covid-19 pindi wanapotembelea vituo vya afya kumeleta changamoto mpya za mapambano dhidi ya Chagas.
Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanatajwa kuwa njia kuu ya kuambukiza ugonjwa wa Chagas. Mauricio Cysne, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Nje katika Unitaid anasema, “ugonjwa wa Chagas huathiri watu milioni 6-7 kwa mwaka kote Amerika Kusini. Ni "ugonjwa wa kimyakimya": unaathiri watu maskini zaidi, walio katika mazingira magumu zaidi na unaua pole pole. Karibu wanawake milioni 2 wa umri wa kupata watoto wanakadiriwa kuathiriwa na Chagas. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni njia kuu ya kuambukiza, kwani ugonjwa huo unakuwa haujagunduliwa au kutibiwa kwa mama na mtoto mchanga.”
Unitaid inatahadharisha kuwa wakati maambukizi mengi bado yanatokea Amerika Kusini, ugonjwa huu unazidi kuenea katika maeneo mengine na maambukizi yanaonekana katika maeneo kama Marekani, Ulaya, Canada, Japan na Australia.