Vurugu nchini Myanmar lazima zikome mara moja: Mashirika ya UN 

12 Aprili 2021

Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Myanmar leo imesisitiza wito wake wa kutaka kukomesha vurugu dhidi ya raia, wakati kukiwa na ripoti za vifo kadhaa katika msako wa hivi karibuni katika maandamano ya kupinga jeshi kushika hatamu. 

Zaidi ya watu 80 walipoteza maisha Ijumaa huku vikosi vya usalama vikiripotiwa kutumia silaha nzito dhidi ya waandamanaji katika mji wa Bago, ulioko karibu kilomita 90 (maili 56) Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu wa kibiashara wa Yangon, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari. 

"Tunafuatilia matukio huko Bago na ripoti za silaha nzito zinazotumiwa dhidi ya raia na kunyimwa matibabu kwa wale waliojeruhiwa", imesema timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo (UNCT) kupitia kwenye ukurasa wake wa Twitter na kusistiza kwamba "Vurugu lazima zikome mara moja". 

Mamia wameuawa 

Mamia ya raia, pamoja na watoto wasiopungua 44, wameuawa katika msako mkali kote Myanmar tangu mapinduzi ya kijeshi kufanyika tarehe 1 Februari.  

Isitoshe wengine wamejeruhiwa vibaya na zaidi ya 2,600 wako kizuizini, wakiwemo wengi walioshikiliwa kwa njia isiyo ya kawaida au kutoweshwa kwa nguvu yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Myanmar. 

Pia kuna ripoti kwamba watu mia kadhaa wamekimbia maeneo yaliyoathiriwa sana na vurugu, wakiwemo wengi ambao wamekimbilia katika nchi jirani. 

Mashirika ya Umoja wa Mataifa pia yameripoti kuongezeka kwa kasi kwa bei ya chakula na mafuta katika maeneo mengi ya nchi hiyo, katika myororo wa usambazaji na ugavi na kusababisha usumbufu wa soko.  

Wataalamu wa misaada ya kibinadamu wana wasiwasi kwamba ikiwa mwenendo wa bei utaendelea, kuwa hivyo "utadhoofisha sana uwezo wa maskini na walio hatarini zaidi kuweza kumudu kuweka chakula cha kutosha kwenye meza za familia zao. 

Mjumbe maalum wa UN ataka suluhu ya mzozo 

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Christine Schraner Burgener, aliwasili Bangkok, Thailand, Ijumaa, kwa ziara ya kikanda kushinikiza juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Myanmar. 

Bi. Schraner Burgener, hata hivyo, hatotembelea Myanmar, alisema kupitia ukurasa wake wa twitter. 

"Ninasikitika kuwa Tatmadaw  (ambalo ni jeshi la Myanmar) limenijibu jana kuwa hawako tayari kunipokea", alisema Mjumbe Maalum akiongeza kuwa 

“Niko tayari kwa mazungumzo. Vurugu hazileti suluhisho la kudumu la amani”. 

Katika mji mkuu wa Thailand, mjumbe huyo maalum amepangwa kukutana na maafisa wa kikanda wa UN na vile vile mabalozi waliothibitishwa kwa Myanmar ambao wako Bangkok. 

Kwa kuongezea  nchini Thailand, mjumbe maalum anashauriana juu ya ziara kwa Jumuiya zingine za Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), na pia nchi zingine za jirani. 

"Kama alivyorejea kusema mara kwa mara, jibu dhabiti la kimataifa kwa mzozo unaoendelea nchini Myanmar linahitaji juhudi ya umoja wa kikanda inayohusisha nchi jirani ambazo zinaweza kuongeza ushawishi wa kuleta utulivu nchini Myanmar", amesema Stéphane Dujarric ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa alipozungumza na waandishi wa Habari hii leo mjini New York. 

Guterres ana hofu kubwa juu ya Myanmar 

Msemaji huyo wa Umoja wa Mastaifa pia amesema Katibu Mkuu anasisitiza wasiwasi mkubwa kuhus kinachoendelea Myanmar.  

Ripoti za hivi punde za vurugu na mauaji ya vikosi vya usalama ni za kutisha ameongeza. 

Baraza la Usalama limetaka wazi wazi kukomeshwa vurugu hizo na kuwaalika wahusika katika mzozo huo kufuata njia ya mazungumzo na maridhiano.  

Katibu Mkuu anahimiza nchi zote wanachama kutumia ushawishi wao kuzichagiza pande husika kuhusu haja ya kukomesha ongezeko hili la machafuko na kuchukua hatua ambazo zitawezesha kurudi kwa utawala wa kiraia.  

Antonio Guterres pia anasisitiza jukumu muhimu ambalo kanda inaweza na lazima ichukue katika kuwashauri watendaji wa kitaifa kuchukua hatua kuelekea kurudi kwa amani na utulivu nchini Myanmar. 

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, Christine Schraner Burgener, kwa sasa yuko katika hiyo, ambapo anakutana na wadau muhimu ili kukuza mwitikio mzuri wa kimataifa kulingana na juhudi za umoja wa kikanda. Anabaki tayari kutembelea Myanmar wakati ambapo fursa itajitokeza. 

Kutoka Myanmar,Dujarric amesema  wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamesema wanashangazwa na ghasia hizo zilizoshika kasi tangu Ijumaa ambapo waandamanaji wengine 93 waliripotiwa kuuawa, wengi wao wakiwa katika mji wa Bago.  

Timu ya UN huko Myanmar inasema ina wasiwasi sana juu ya ripoti za utumiaji wa silaha kali dhidi ya waandamanaji. 

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa upande wake inasema kuwa, hadi leo, ripoti za kuaminika zinaonyesha watu wasiopungua 707 wameuawa tangu jeshi lilipotwaa madaraka  zaidi ya miezi miwili iliyopita. Inaaminika kuwa na idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi. Tangu Februari 1, maelfu ya watu wamejeruhiwa, wengi wao vibaya. 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter