Sudan tekelezeni mpango wa kitaifa wa ulinzi wa raia kuepusha kinachoendelea Darfur Magharibi- OHCHR 

9 Aprili 2021

Ofisi ya kamishna wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, OHCHR, imeshtushwa na ripoti za hivi karibuni za kuibuka kwa mapigano kati ya makabila ya Masalit na waarabu huko El Geneina jimboni Darfur Magharibi nchini Sudan. 

Msemaji wa OHCHR mjini Geneva, Uswisi, Marta Hurtado amewaambia waandishi wa Habari hii leo kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu wapatao 87 huku wengine zaidi ya 191 wamejeruhiwa na maelfu wamelazimika kukimbia makazi yao. “Mapigano hayo mapya yameibuka tarehe 3 mwezi huu wa Aprili huko El Geneina baada ya watu wasiojulikana kufyatulia risasi kundi la wanaume wa kabila la Masalit, na kuua wawili na kumjeruhi mmoja wao. Katika kujibu mashambulizi, watu waliojihami kutoka makabila ya Masalit na waarabu walihamasishana na kusababisha mapigano baina yao. Ilipofika jioni ya tarehe 5, mitaa ya Al Geneina ilikuwa imefurikwa na miili, ikiwemo ya wanawake na watoto. Matukio haya yanakumbushia taswira ya kilichotokea Darfur Magharibi kufuatia mapigano ya mwishoni mwa mwaka 2019 na hivi karibuni zaidi mwezi Januari mwaka 2021.” 

Bi. Hurtado amesema hali kama hiyo ya mapigano zimeripotiwa katika eneo hio la Al Geneina na mamlaka zimeshindwa kudhibiti licha ya kuwepo kwa ulinzi wa kutosha mjini humo. 

Amesema OHCHR inatoa wito kwa serikali ya Sudan kuharakisha utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa ulinzi wa raia. 

Bi. Hurtado amesisitiza kuwa makabila yote yanayowajibika na ghasia zinazotokea Darfur yanapaswa kusalimisha silaha na serikali iweze kusimamisha utulivu na kuhakikisha utawala wa sheria ikiwemo kuzuia raia kuvunja sheria. 

Halikadhalika ofisi hiyo inasihi serikali ichunguze haraka tukio hilo kwa uwazi na bila kuegemea upande wowote. 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter