Sasa ni mbio za kupata medali Tokyo badala ya mbio za kujinusuru- UNHCR 

7 Aprili 2021

Kuelekea michezo ya majira ya joto ya olimpiki mwaka 2020 itakayofanyika huko Tokyo Japan kuanzia mwezi Julai mwaka huu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limezindua kampeni ya #TheJourney au safari kwa ajili ya kusaidia timu ya wanamichezo wakimbizi watakaoshiriki mashindano hayo na yale ya watu wenye ulemavu

Ndivyo inavyoanza video ya kampeni hiyo ya kuchangia wanamichezo wakimbizi watakaoshiriki michezo ya olimpiki! 

Mtu anaonekana akihaha kukusanya virago vyake kubeba hiki na kile awezacho, huku nje milio ya risasi ikisikika, na watu wengine wakionekana wakihaha kujinusuru maisha yao kuelekea pahala salama zaidi. 

Ni kukimbia na kuanguka na hatimaye anapata jeraha kwenye goti! Anafunga kitambaa na kuendelea na safari yake.. huku akichechemea.. 

 Njia nako masahibu ni mengi, akishuhudia wenzake wakikamatwa, huku yeye akijificha …. Na kisha kuendelea na safari katikati ya hofu kubwa mchana na usiku! 

Hatimaye anapanda boti kwenye safari ambayo si salama, maisha yake akiweka rehani! Baada ya kuwasili ugenini, maisha ni magumu, analala nje, baridi ikiwa ni kali…bila viatu na hata matandiko! 

Msaada wa raba za kuvaa unamfungulia njia ya kuanza kufanya mazoezi na kukimbia!!! 

Na kisha mkimbizi huyu anajiunga na timu ya wakimbizi watakaoshiriki michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 inayofanyika mwaka huu baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na Covid-19. 

Sasa UNHCR kupitia kampeni ya #TheJourney inasihi michango kuwezesha wanamichezo hawa ambao sasa hawakimbii tena kusaka usalama bali wanakimbia kujenga utangamano, umoja na zaidi ya yote kupata medali! 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter