Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulimwengu uzingatie tulichojifunza kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda 

Mnara wa kumbukizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya waTutsi nchini Rwanda mwaka 1994 ikizunduliwa mjini Geneva kwenye Umoja wa Mataifa.(maktaba)
UN Photo/Violaine Martin
Mnara wa kumbukizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya waTutsi nchini Rwanda mwaka 1994 ikizunduliwa mjini Geneva kwenye Umoja wa Mataifa.(maktaba)

Ulimwengu uzingatie tulichojifunza kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda 

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa kuadhimisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Tafakari kuhusu Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 Dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.alioutoa kwa njia ya video, amesema wakati huu dunia inapojiunga katika mshikamano na watu wa Rwanda, ni lazima kuangalia sana ulimwengu wa leo na kuhakikisha kwamba tunazingatia masomo ambayo wanadamu waliyapata kutokana na tukio hilo la miaka 27 iliyopita ambapo zaidi ya watu milioni moja waliuawa.  

“Leo, kote ulimwenguni, watu wanatishwa na vikundi vyenye msimamo mkali vilivyoazimia kuongeza vyeo vyao kupitia mgawanyo wa kijamii na ulaghai wa kisiasa na kitamaduni. Harakati hizi zenye msimamo mkali zinawakilisha tishio kuu la usalama katika nchi nyingi. Wakati teknolojia na mbinu wanazotumia wenye itikadi kali zinabadilika, ujumbe mbaya na kejeli vinabaki vile vile. Kuziondolea utu jamii, habari potofu na matamshi ya chuki yanachochea moto wa vurugu.” 

Bwana Guterres akiendelea kusisitiza kuhusu umuhimu wa ulimwengu wa leo kujifunza kutokana na historia, amesema, 

Tweet URL

“tuliona kile kilichotokea Rwanda mnamo 1994, na tunajua matokeo mabaya wakati chuki inaporuhusiwa kutamalaki.” 

Katibu Mkuu Guterres akieleza namna Rwanda ilivyoweza kupona na kuibuka tena kutoka katika maumivu na madhara ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, amesema,“baada ya kukumbwa na unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia ambao hausemeki, wanawake wa Rwanda sasa wanashikilia zaidi ya asilimia 60 ya viti vya bunge na kuifanya Rwanda kuwa kiongozi wa ulimwengu. Watu wa Rwanda wametuonesha nguvu ya haki na upatanisho, na uwezekano wa maendeleo. Katika Siku hii adhimu, sote tujitolee kujenga ulimwengu unaoongozwa na haki za binadamu na hadhi kwa wote.” 

Mwaka huu ni miaka 27 tangu zaidi ya watu milioni moja waliuawa kwa utaratibu maalumu chini ya miezi mitatu nchini Rwanda. Kwa kiasi kikubwa waliouawa walikuwa Watutsi, lakini pia Wahutu na wengine ambao waliopinga mauaji ya kimbari.