Jitihada za Afrika dhidi ya mabadiliko ya tabianchi inabidi zifadhiliwe zaidi - Guterres

6 Aprili 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres hii leo Jumanne amesema jitihada za Afrika za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinahitaji kuharakishwa na hii inahitaji msaada wa kifedha kutoka kwa ulimwengu ulioendelea.  

Bwana Guterres ameyasema hayo wakati wa mjadala  kuhusu janga la Covid-19 na dharura ya mabadiliko ya tabianchi ambavyo vinaliathiri bara la Afrika. Mazungumzo hayo yameandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB. 

Ili kufanikisha hili, Katibu Mkuu Guterres ameweka mapendekezo matano ambayo ni: 

Kwanza, ametoa wito kwa washiriki wote wa mataifa ya G7 na nchi nyingine zilizoendelea, pamoja na benki za maendeleo za kitaifa, kuongeza sehemu ya fedha za mabadiliko ya tabianchi zilizotengwa kwa marekebisho na mnepo kwa angalau 50%. ya jumla ya fedha yao waliyoitenga kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi. Guterres amesema kwa sasa kiwango cha ufadhili ni asilimia 20.  

Pili, serikali zote na wafanyabiashara kuingiza hatari za mabadiliko ya tabianchi katika sera na maamuzi ya uwekezaji, pamoja na bajeti na ununuzi. “Nchi zinazoendelea lazima zipewe zana na njia za kufanikisha hili. Sahihi na habari mpya za hatari ni hatua ya kwanza muhimu katika usimamizi bora wa hatari, " Amebainisha Bwana Guterres. 

Tatu, Afrika inastahili uwekezaji zaidi. 

Nne, Katibu Mkuu anaamini kuwa wadau wa ushirikiano wa kimataifa wanapaswa kuongeza msaada wao kwa mipango ya kukabiiana na hali pamoja na mnepo, kama vile ‘mkakati wa ukuta wa kijani’ pamoja na kamati ya Bonde la Sahel na Congo.  

Mwisho, Bwana Guterres ametoa wito kwamba na Mkutano ujao wa Mabadiliko ya Tabianchi , COP26 huko Glasgow mnamo Novemba mwaka huu, mapendekezo halisi yatawekwa mezani ili kufanya ufikiaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi uwe rahisi na haraka, kwa kujumuisha na mataifa ya Afrika. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter