Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya COVID-19 yaondoa hofu kwa wahudumu wa afya Uganda 

Nchini Uganda chanjo zinasafirishwa kwa kutumia miguu, boti au piki piki.
© UNICEF/Henry Bongyereirwe
Nchini Uganda chanjo zinasafirishwa kwa kutumia miguu, boti au piki piki.

Chanjo dhidi ya COVID-19 yaondoa hofu kwa wahudumu wa afya Uganda 

Afya

Ugonjwa wa Corona au COVID-19 ulizua zahma kubwa duniani ulipoibuka mwaka jana na kuleta sintofahamu. Hali hiyo bado haijaisha hadi sasa ambapo ni mwaka mmoja umeshapita na watu zaidi ya milioni 128 wameugua duniani kote hadi sasa na kati yao hao zaidi ya milioni 2.8 wamefariki dunia. 

Bado mazuio ya safari yamewekwa katika baadhi ya nchi na masharti ya kujikinga kwa kuvaa barakoa, kuepuka michangamano na kutumia vitakasa mikono zinazingatiwa. Hata hivyo chanjo imepatikana na inaleta nuru. Siyo tu kwa wananchi wa kawaida bali pia kwa wahudumu wa afya ambao nao waliingiwa na hofu . 

Miongoni mwa wahudumu waliokumbwa na hofu ni wale wa nchini Uganda ambako uzinduzi wa utoaji chanjo dhidi ya COVID-19 ulifanyika tarehe 10 mwezi uliopita wa Machi katika hospitali ya rufaa ya Mulago jijini Kampala.  

Winifred Viola Baluka, muuguzi katika kituo cha afya cha Kisenyi jijini Kampala ambaye anasema, “Hii ilipokuja, kuna wakati unahisi kuhofia na wakati huo nilikuwa mjamzito. Na kuna wakati nikahofu pengine mtoto wangu aliye tumboni anaweza kuwa hatarini iwapo nitapata virusi vya Corona. Hofu kubwa ilikuwepo lakini cha msingi nilizingatia kanuni za afya na kuendelea kuhudumia wagonjwa.” 

Soundcloud

 

Ujio wa chanjo ukawa nuru kwa Winifred akisema, “Haswa! Nimepata dozi ya kwanza ya chanjo, sijapata shida yoyote. Unafahamu chanjo mpya inapoingia, ni kama chanjo zingine zozote, kawaida kunakuwepo na mtazamo hasi kutoka kwa wahudumu wa afya, jamii lakini ni vyema kwetu sisi kuishi kwa mfano, kwa kupatiwa chanjo..” 

Hata hivyo muuguzi huyu akaenda mbali zaidi akisema, “Kwa kuwa nimepata dozi yangu ya kwanza, haimaanishi kuwa sasa nina kinga kamili! La hasha! Ninahitaji kupata dozi ya pili, kwa hiyo nitaendelea kujikinga kwa kuzingatia kanuni za utendaji, lakini nina furaha. Nitaendelea kushawishi wengine nao wapate chanjo kadri chanjo zitakavyoendelea kuletwa.” 

Akiangazia shaka na shuku iliyokuwepo awali, Profesa Seggane Musisi, Mkuu wa Idara ya magonjwa ya akili kwenye Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda anasema, “Jambo muhimu zaidi ni kutambua kuwa huu ulikuwa ugonjwa mpya kabisa. Ugonjwa uliotisha mno, unaambukiza, unaua na unakuathiri kwa njia ambayo ni vigumu sana kujikinga. Hatukuuelewa vizuri. Mwanzoni ulileta hofu kubwa kwenye jamii na bila shaka kwa wahudumu wa afya na wao kwa kuwa ni binadamu walihofia ziadi kwa sababu walifahamu walipaswa kushughulikia ugonjwa hatari mno, unaoweza kuwapata na kuwaua.” 

Akamulika zaidi mfumo wa afya ulivyozidiwa uwezo kutokana na COVID-19 akisema,“Hospitali zilijaa na baya zaidi, Corona ilijengea hofu wale ambao tayari walikuwa mahututi na magonjwa kama vile saratani, kisukari, shinikizo la damu bila kusahau madaktari na wahudumu wa afya wazee.” 

Na sasa chanjo dhidi ya Corona ni nuru gizani akisema, “Jambo la kwanza ni ile hali ya kuona  unafuu. Wenzetu wengi wamefariki dunia kutokana na Corona lakini sasa unahisi kuwa umeshapata chanjo ya kwanza ya kukabili ugonjwa na hivyo unaweza kwenda kuhudumia wagonjwa wako bila uoga wowote wa kuweza kuambukizwa, au hofu ya kuwa una ugonjwa na hivyo kuwaambukiza. Kwangu mimi ni jambo zuri na nasubiri kwa hamu dozi ya pili ili niwe kamilifu. Kwa hiyo sasa tuna uhakika wa chanjo kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa.” 

Dkt. Noeline Nakasuga wa Idara ya magonjwa ya akili katika hospitali ya Mulago anamulika vile ambavyo wagonjwa wa akili walihaha wakati Corona ilipoingia. Dkt. Nakasuga anasema, “Kama huduma zingine zilivyoathirika wakati wa zuio la usafiri, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa wagonjwa wa akili kwa sababu walishindwa kufika hospitali kupokea dawa zao licha ya kwamba hospitali ilikuwa wazi. “ 

Na sasa chanjo imepatikana na imefika Uganda ni fursa nzuri kwa kuwa, “Kwa kweli nimepata chanjo hii ili watu wengine wafahamu kuwa ni salama na inajenga matumaini ya kwamba kuna hatua inaweza kuchukuliwa dhidi ya ugonjwa huu wa kutisha na matumaini ya kwamba hatimaye tunaweza kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huu, ingawa haimaanishi eti hivi sasa barakoa tuzitupe na tuchangamane. Inatupa matumaini ya kuwa siku moja tunaweza kurejea katika hali ya kawaida ya kuchangamana.”