Walinda amani 4 wa UN wauawa Mali, 19 wajeruhiwa, Guterres azungumza
Walinda amani 4 wa UN wauawa Mali, 19 wajeruhiwa, Guterres azungumza
Walinda amani wanne wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu nchini Mali wameuawa kwenye kambi yao huko Aquelhok jimboni Kidal, huku wengine 19 wamejeruhiwa, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Walinda amani hao ni raia wa Chad.
Shambulio hilo limetokea leo Ijumaa ambapo Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stephane Dujarric, amelaani vikali akisema shambulio lolote dhidi ya walinda amani linaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa, na vikwazo vinaweza kuwekwa dhidi ya wote waliohusika.
Amekumbusha kuwa mamlaka za Mali zifanye jitihada zote katika kubaini na kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa shambuli hilo la kikatili.
Shambulio limefanywa na magaidi walio na silaha nzito
Shambulio hilo yaelezwa limetokea saa 12 na dakika 15 asubuhi ya Mali ambapo helikopta zilipelekwa kwenye eneo la tukio ili kuokoa majeruhi.
Kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, walinda amani wanaohudumu chini ya ujumbe huo kwa kwa ujasiri waliweza kudhibiti na kuwafurusha magaidi waliokuwa na silaha nzito, “na washambuliaji kadhaa waliuawa,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa kwa lugha ya kifaransa.
MINUSMA imelaani vikali shambulio hilo ikieleza kuwa ni jaribio lingine linalofanywa na maadui wa amani, dhidi ya mchakato wa amani na utekelezaji wa mkataba wa amani.
Naye Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, kupitia mtandao wa Twitter amelaani vikali shambulio hilo akisema, “uhalifu huo lazima uadhibiwe.”
Guterres, MINUSMA na Lacroix wametuma salamu za rambirambi kwa serikali ya Chad, na familia za walinda amani waliouawa huku wakiwatakia ahueni ya haraka na uponaji wa mapema majeruhi wote.
Katibu Mkuu pia amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na wananchi wa Mali katika harakati zao za kusaka amani ya kudumu.
MINUSMA imekuwepo nchini Mali tangu mwaka 2013 kufuatia mapinduzi ya kijeshi na kutwaliwa kwa eneo la kaskazini mwa Mali na waislamu wenye misimamo mikali.
Ujumbe huo unaunga mkono utekelezaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2015, uliotiwa saini na mamlaka na usharika wa vikundi viwili vilivyojihami na inachukuliwa kuwa Mali ni eneo hatari zaidi kwa operesheni za Umoja wa Mataifa.