Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde ambao hamjaridhia mkataba wa kutokomeza mabomu fanyeni hima- Guterres

UNMAS wakitegua mabomu katika eneo la Equatoria mashariki nchini Sudan Kusini
UNMISS\Nektarios Markogiannis
UNMAS wakitegua mabomu katika eneo la Equatoria mashariki nchini Sudan Kusini

Chonde chonde ambao hamjaridhia mkataba wa kutokomeza mabomu fanyeni hima- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja huo ambazo bado hazijatia saini na kuridhia mkataba wa kimataifa wa kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini na vilipuzi, zifanye hivyo haraka ili hatimaye kuondokana na mabomu hayo yanayoua na hata kuacha binadamu na ulemavu wa kudumu.

Bwana Guterres amesema hayo hii leo katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu madhara ya mabomu hayo sambamba na kusaidia hatua za kuyaondoa kule ambako bado yamesalia.

"Zaidi ya nchi 160 ni wanachama wa mkataba wa kimataifa wa kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini. Natoa wito kwa nchi ambazo bado haziijasaini mkataba huo zifanye hivyo bila kuchelewa. Siku ya leo inatupatia fursa ya kutafakari safari yetu ya kuongeza uelewa kuhusu hatari za mabomu ya kutegwa ardhini na kuahidi tena juu ya malengo yetu ya kuwa na dunia isiyo na mabomu hayo," amesema Katibu Mkuu kwenye ujumbe wake.

Amefafanua kuwa mabomu ya kutegwa ardhini, masalia ya mabomu na vilipuzi vinavyotumika vitani na vile vinavyotengenezwa kiholela vinaathiri watu walio hatarini zaidi, wakimbizi, waliofurushwa na watoto na zaidi ya yote, "vinakwamisha suluhu za kuleta amani, hatua za kibinadamu na ni kikwazo cha maendeleo endelevu na jumuishi."

Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS
UNMAS
Suzan Kiden Dominic, mteguaji mabomu aliyefundishwa na UNMAS

Bwana Guterres amesema kwa bahati mbaya, hatua zinapigwa katika kuondoa na kutegeua mabomu hayo lakini baadaye yanarejeshwa. "Lakini hatuwezi kuridhika na uchechemuzi na kampeni za kuongeza uelewa wa hatari zitokanazo na mabomu ya kutegwa ardhini. Chata ya Umoja wa Mataifa inatutaka tukamilishe kazi."

Kazi hiyo ni kutafiti, kusafisha na kuharibu vilipuzi hivyo hatari na ndipo akatamatisha ujumbe wake akisema, "hebu na tufanye huu kuwa muongo wa mwisho tunaohitaji katika kuazimia tena kukamilisha kazi hii."

 Mkataba wa kimataifa wa kuondokana na mabomu ya kutegwa ardhini na vilipuzi au mkataba wa Ottawa, ulianza kutumika tarehe 1 mwezi Machi mwaka 1999.

Mchechemuzi wa kimataifa Daniel Craig naye azungumza

Naye Daniel Craig ambaye ni mchehemuzi wa kimataifa kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini ameongeza sauti yake kwenye siku hii ya le.

Katika ujumbe wake amesema, "nimefurahia sana kuongeza sauti yangu leo kwa ile ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na viongozi wengine wengi, wanaharakati, na raia wanaojali, kutoa wito kwa mataifa yote kuelekeza nguvu zao kwenye lengo la mwisho la kuondokana na ulimwengu wenye mabomu ya ardhini na mabaki ya vilipuzi vya vita. Inahitaji kuchukua uamuzi."

Baada ya kupata mafunzo kutoka UNMAS, walinda amani hawa kutoka Cambodia kwenye kikosi cha MINUSMA wako tayari kutegua mabomu na vilipuzi.
UN /Marco Dormino
Baada ya kupata mafunzo kutoka UNMAS, walinda amani hawa kutoka Cambodia kwenye kikosi cha MINUSMA wako tayari kutegua mabomu na vilipuzi.

Craig amesema wakati dunia inachomoza kutoka kwenye kivuli cha janga la Corona, "nataka kuwasifu wanaume na wanawake ambao waliendelea na jukumu lao la kusafisha na kuharibu mamia ya maelfu ya vilipuzi mwaka 2020, kuanzia mabomu ya kutegwa ardhini, hadi mabomu ambayo hayajalipuka na vifaa vya milipuko. Kazi iliendelea kwa sababu watu binafsi, mashirika na serikali waliishikilia."

Bomu moja la kutegwa ardhini linaweza kusambaratisha jamii: kuua baba, mama, na mara nyingi mtoto- Daniel Craig, Mchechemuzi wa kimataifa

Amesema uwanja mpya na salama ulijengwa nchini Kambodja, huku Chile ikitangaza kuwa eneo lake liko huru bila mabomu, na nchi zote wanachama wa mkataba wa kupiga marufuku mabomu zimetangaza nia yao ya kusafisha katika nchi zao mabomu ya ardhini ifikapo mwishoni mwa muongo huu.

Bado kuna uchafuzi utokanao na mabomu

Hata hivyo amesema kuna uchafuzi mpya. "Mwezi uliopita tuliadhimisha miaka 10 ya vita huko Syria, mzozo ambao umesababisha mamia ya maelfu ya vifo, mamilioni ya wakimbizi na maelfu ya tani za uchafuzi mpya wa vilipuzi. Mapigano yanahitaji kukoma. Na usafishaji uanapaswa kuanza mapema iwezekanavyo na kwa kasi."

Na kuna uchafuzi wa zamani. Vita vya Vietnam vilimalizika rasmi zaidi ya miaka 45 iliyopita, lakini mabomu ya ardhini na mabaki ya vilipuzi bado yanaathiri maeneo mengi. "Bomu moja la kutegwa ardhini linaweza kusambaratisha jamii: kuua baba, mama, na mara nyingi mtoto" amesema Craig.

Amesisitiza kuwa dira inayopaswa kujitahidi kuifikia ni ulimwengu ambamo watu na jamii wanaishi katika nyumba salama, kwenye viwanja salama, kwenye mazingira salama. Ambamo haki za binadamu, haki ya kuishi, uhuru, ulinzi binafsi na mahitaji ya msingi yanatimizwa na hakuna mtu yeyote aliyeachwa nyuma, wakiwemo manusura wa ajali za milipuko, wale waliojeruhiwa na kulemazwa, ambao lazima wajumuishwe kikamilifu kama wanachama sawa wa jamii zao.