Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yafanikisha kuwapa hifadhi tena wakimbizi wa Mali waliofurushwa katika kambi Burkina Faso 

Wanawake wakimbizi wakichota maji mji wa Djibo nchini Burkina Faso.
UNOCHA/Naomi Frerotte
Wanawake wakimbizi wakichota maji mji wa Djibo nchini Burkina Faso.

UNHCR yafanikisha kuwapa hifadhi tena wakimbizi wa Mali waliofurushwa katika kambi Burkina Faso 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR baada ya kuweka mazingira mazuri ya kurejea kwa wakimbizi wa Mali waliokuwa wamevikimbia vitisho na mashambulizi katika kambi mbili za nchini Burkina Faso, shirika hilo hivi karibuni liliratibu kuhamishwa kwa wakimbizi wapatao 1,211 kutoka Djibo kwenda kambi ya Goudoubo.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, inawaonesha wakimbizi wa Mali wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Goudoubo ambayo kwa wengi wao wanaona hapo ndipo nyumbani kwao. Miongoni mwao ni Fatimata na pacha wake ambao wana umri wa miaka 70. Fatimata anasema, “tangu utoto wetu na sasa ukimbizini, tunaishi vizuri pamoja.” 

Mapacha hawa walikimbia Mali kwa mara ya kwanza mwaka 2013. Mdogo wao wa kike akawafuata mwaka 2019 kwa sababu ya kukosekana kwa usalama.  

Mdogo wao huyo anaitwa Ramata, anasema, “wote tulikimbia kwa sababu hiyo hiyo.”  

Kote Sahel, usalama ni mgumu kupatikana. Mwaka mmoja uliopita, wakimbizi 9,000 wa Mali waliikimbia Kambi ya Goudoubo kwa sababu ya vitisho. Mnamo mwaka wa 2020, UNHCR iliijenga tena kambi hiyo, na kuweka makazi mapya 1,500. Usalama uliimarishwa na maelfu ya wakimbizi wamerudi. 

Familia ya mapacha hawa ambayo sasa ni vizazi vinne, watu 30 ambao si mara moja au mbili wamefurushwa akiwemo mpwa wao Aissata ambaye anasema, “nina furaha hapa. Kuna amani na ninatapokea usaidizi.” 

Zaidi ya wakimbizi 6,500 wamerejea kambini hapa hadi sasa. Hapa watapata maji, mahali pa wanyama wao na huduma za afya. 

Kambi ya Goudoubo ilikuwa ikiwahifadhi wakimbizi 9,000 hadi Machi mwaka jana wakati mfululizo wa mashambulio ya vurugu na mauaji yaliyotekelezwa na watu wenye msimamo mkali yaliwalazimisha  wakimbizi wote kuikimbia kambi hiyo.