Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni tete Cabo Delgado, mashirika ya UN yahaha kunususu raia

Takriban watu 700,000 wamefurushwa kufuatia ukatili jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.
UNDP/Cláudia Fernandes
Takriban watu 700,000 wamefurushwa kufuatia ukatili jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Hali ni tete Cabo Delgado, mashirika ya UN yahaha kunususu raia

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti kuwepo kwa mashambulizi dhidi ya raia kwenye mji wa Palma jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji na kusababisha maelfu ya watu kukimbilia maeneo ya jirani ikiwemo mpakani na Tanzania.

Mashirika hayo lile la uhamiaji, IOM, mpango wa chakula duniani , WFP,  ofisi ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR,  yamesema makumi kadhaa ya watu wameuawa wakati wa mashambulio hayo kutoka kwa waasi waliojihami ambao yaripotiwa waliingia mjini humo mwishoni mwa wiki. 

Msemaji wa OCHA, Jens Laerke amesema kile kinachoendelea Palma ni ukatili dhidi ya raia kutoka kwa makundi yaliyojihami yasiyo ya kiserikali, “na ndio maana nasema wamefanya vitendo vya kikatili, wanaendelea kufanya na tumepata ripoti mashambulizi yanaendelea na tunazungumzia uwezekano wa watu zaidi kukimbia wilaya ya Palma kuelekea maeneo mengine ikiwemo mpakani na Tanzania.” 

Paul Dillon ambaaye ni msemaji wa IOM amefafanua kuwa hadi jana tarehe 30 mwezi Machi, watu 3,361 ambao ni familia 672 wamesajiliwa na IOM na kwamba, “watu hao wanawasili wilaya za Ulongwe, Mueda, Montepuez na Pemba wakitokea  Palma kwa mguu, mabasi na  ndege.” 

Kwa upande wake UNHCR inasema familia zimekimbia ghasia na zinasaka hifadhi misituni huku zaidi ya watu 100 wamesafiri kwa boti kutoka Palma hadi Pemba. 

Tangu mashambulizi dhidi ya raia yaanze huko Cabo delgado mwezi Oktoba mwaka 2017, zaidi ya watu 670,000 wamekimbia makwao, imesema IOM huku nusu yao wakiripotiwa kuwa ni watoto wanaohitaji msaada wa dharura. 

Likiangazia athari za mashambulizi hayo kwa raia, UNHCR kupitia msemaji wake Andrej Mahecic imesema watu wanauawa, wanakatwa viungo, mali zao zimeporwa na mashamba yameharibiwa. 

“Watu wamefukuzwa kwenye nyumba zao wakiwa na virago vichache mno. Wanawake na watoto wa kike wanatekwa na kulazimishwa kuolewa, katika matukio mengine visa vya kubakwa au aina nyingine ya ukatili wa kingono vimeripotiwa. Huku kukiweko ripoti pia za watoto kutumikishwa na waasi waliojihami.” 

WFP Pamoja na kwamba imeshasambaza misaada ya tani 250 ya chakula kwa watu 16,000 huko Palma, bado inasema msaada zaidi umesitishwa kutolewa kutokana na ghasia zinazoendelea, ingawa wahudumu wa afya imebidi wapelekwe ili kutoka huduma za dharura kwa majeruhi na wenye uhitaji zaidi.