Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa IFAD umeniokoa mimi na familia yangu: Mjasiriamali Fatou 

Mwanamke akichuuza mbogamboga nchini Gambia.
FAO/Seyllou Diallo
Mwanamke akichuuza mbogamboga nchini Gambia.

Msaada wa IFAD umeniokoa mimi na familia yangu: Mjasiriamali Fatou 

Ukuaji wa Kiuchumi

Duniani kote mamilioni ya wasichana na wanawake vijijini wanaweza kuendesha maisha yao kwa kutumia ardhi inayowazunguka, lakini mara nyingi wanashindwa kufanya hivyo kwa ukosefu wa mtaji wa kuanzia kutekeleza malengo yao, Sasa mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD unashirikiana na serikali mbalimbali kutoa mitaji inayowawezesha wasichana kuingia katika bishara ya kilimo kama  alivyofanya Fatou Secan nchini Gambia.

Fatou Jaw Secan mwenye umri wa miaka 24 ni mjasiriamali wa kilimo cha mbogamboga na anaishi katika Kijiji cha Kombo Darslami. Je alianzaje kilimo hicho cha mbogamboga? 

“Mama yangu alikuwa ananichukua alipokuwa akienda shamba kulima, hivyo nimekuwa nacho kilimo hadi pale nilipobaini thamani yake” 

Fatou ana kipande chake cha ardhi katika bustani ya mbogamboga ya jamii ya vijana wa Darslami  ambayo ni sehemu ya mradi wa IFAD ujulikanao kama NEMA wenye lengo la kuwasaidia wakulima zaidi ya 20,000 waende sanjari na mifumo endelevu  ya uzalishaji na kuboresha ujuzi wao wa biashara. 

Fatou alibahatika kuingia katika mradi huo uliomwezesha kupata mtaji wa kuanzia biashara yake ya kilimo cha mbogamboga ,“Baada ya muda nilifanikiwa kupata majaruba 11 katika mradi wa bustan wa NEMA ambao ulianzishwa ili kuchagiza uwezeshaji wa wanawake katika Kijiji cha Kombo Darslami. Nyumbani kwetu wote, kila mtu alikuja katika bustani hii na wote tumefaidika nayo na kuoana thamani tunayoipata kutokana na bustani hii” 

Kwa sababu Fatou anauza mboga zake kwa jumla bishara yake inakua na sasa kila siku anapeleka mazao yake sokoni, pia anajaribu kutafuta bei za masoko na kuwachagiza wanawake wengine kuingia katika biashara hiyo ambayo kwa miezi saba aliyofanya hadi sasa, anasema imemsadia kulipa deni lake la karo ya shule, kulipia mafunzo ya kompyuta ambayo yatamfaa siku za usoni, kulipia wadogo zake karo na pia kuwasaidia wazazi wake.