UNICEF yawezesha mtoto mkimbizi kuwa na ndoto ya kuwa daktari 

30 Machi 2021

Nchini Niger watoto wakimbizi waliolazimika kukimbia Libya kutokana na ghasia za ugenini hivi sasa wanaona nuru ya maisha yao baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNICEF, kuwapatia maeneo salama siyo tu ya kucheza bali pia kujifunza. 

Miongoni mwa watoto hao ni Wichah Nasradine, mtoto mwenye uraia wa Sudan, akiwa Agedez nchini Niger, na ana umri wa miaka 13. 

Wichah hivi sasa yuko ukimbizini kwenye nchi ya tatu, Niger akisema, “tulikimbia nchi yetu Sudan kwa sababu ya vita. Tulikimbilia Libya, ambako nako tumekimbia kwa sababu ya vita. Nchini Libya tulisikia milio mizito ya risasi. Mama yetu alituficha nyumbani. Tuliwasili hapa Niger mwaka 2018 ili kusaka hifadhi. Ili kusahau vita tunatoka kucheza nje, nacheza pia na kaka zangu.” 

Wichah ambaye ana ndugu wanne ambao ni kaka na dada zake, anasema siku moja walitaka mtoto mmoja mwakilishi wa watoto, na ndipo walimchagua yeye. 

Wichah anakwenda shuleni na anasema yeye ni mwakilishi kwa hiyo huzungumzia elimu kwa kuwa shule ni muhimu na ndio ufunguo ambao unaweza kutumia kufungulia kila kitu maishani.  Mtoto huyu anaendelea kusema kuwa darasani wana mwalimu mmoja anayewafundisha lugha ya kifaransa. 

Tayari Wichah ameandikishwa darasa la kwanza na anasema ya kwamba, “shuleni kwake ana marafiki kutoka Niger amao wanasoma na kucheza pamoja.” 

Na zaidi ya yote, Wichah ana ndoto na anasema “nikiwa mkubwa nataka kuwa daktari ili niweze kutibu wagonjwa.” 

Kwa mujibu wa UNICEF, vita vya wenyewe kwa wenyewe vimefurumusha zaidi ya watoto milioni 30. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter