Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumekuwa na mafanikio lakini bado tunajikongoja kufikia usawa wa kijinsia:Guterres 

Lago Mayor de Chapultepec, Mexico City.
UN-Habitat)
Lago Mayor de Chapultepec, Mexico City.

Kumekuwa na mafanikio lakini bado tunajikongoja kufikia usawa wa kijinsia:Guterres 

Wanawake

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema miaka 26 baada ya mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake na usawa wa kijinsia , hatua kubwa zimepigwa na mafanikio yameonekana lakini bado dunia inajikongoja kutimiza azimio la Beijing na hatua za kufikia usawa wa kijinsia. 

Katika hotuba yake kwenye kongamano la kizazi cha usawa lililoanza leo Mexico City mji mkuu wa Mexico kwa njia ya mtandao Antonio Guterres amersema, “wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, masuala ya kijinsia na vijana kote ulimwenguni wameendelea kusongesha mchakato wa kufikia lengo la usawa, kuilainisha mifumo dume iliyokita mizizi, kubadili baadhi ya mila na desturi na kuhamisha madaraka na kuwapa wale ambao mara nyingi husahaulika na kunyamazishwa, kumekuwepo na ushindi mkubwa lakini mchakato unakwenda polepole mno na huu ni wakati wa kubadili hilo.” 

Usawa wa kijinsia ni suala la mamlaka 

Bwana Guterres ameongeza kuwa usawa wa kijinsia ni suala la mamlaka na mamlaka yanasalia mikononi mwa wanaume. 

Amesema, “katika maeneo mengi, wazo la usawa wa kijinsia limeshambuliwa. Sheria za ukandamizaji zimerudi, na unyanyasaji wa kutisha dhidi ya wanawake unaongezeka, mambo ambayo ninayalaani kabisa. Na sasa, mshituko wa janga la COVID-19 umehjarubu na kusambaratisha maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana na kuathiri hatua za mafanikio yetu mengi tuliyopata.” 

 Katibu mkuu akaenda mbali zaidi na kuisitiza kwamba “ Huu ni wakati wa kujikusanya na kujipanga tena kwa ajili ya kutimiza azma yetu kuunda ulimwengu ulio sawa, wa haki, na endelevu zaidi ambao watu wote wanaweza kutambua haki zao za binadamu bila ubaguzi na bila woga. Na kazi hii ni ya wanawake wote.” 

 Amesema ni kwa kina mama wote kila mahali, “ambao wanahaha kujumuisha masuala ya kikazi na mzigo mkubwa unaoongezeka wa kutoa huduma, kwa washichana kutoka jamii za asili na watoto wakimbizi, kwa mwanamke anayeishi na ulemavu au anayesaka ajira katika masuala ya teknolojia na sayansi, kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu na wengine wengi. Kazi hii ni kwa ajili ya wote na lazima ifanywe na wote wanawake na wanaume vilevile.” 

Hatua za kuchukua tunapojikwamua na COVID-19 

Tunapojikwamua kutoka kwa janga la COVID-19 Katibu Mkuu amesisitiza kwamba ni, lazima tuzingatia hatua tano muhimu: 

Kwanza, linda haki sawa za wanawake na ufute sheria za kibaguzi. 

Pili, hakikisha uwakilishi sawa kuanzia katika bodi za kampuni hadi mabunge na zaidi kupitia hatua maalum na nafasi za upendeleo. 

Tatu, ongeza ujumuishaji wa wanawake kiuchumi kupitia malipo sawa, ulinzi wa kazi, mikopo inayolengwa na uwekezaji katika uchumi wa huduma na hifadhi ya jamii. 

Nne, mara moja weka mipango ya hatua za dharura kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. 

Tano, toa nafasi kwa kipindi cha mpito cha kizazi kinachoendelea na kwa vijana ambao wanatetea ulimwengu ulio na haki zaidi na sawa. 

Ameongeza kuwa, “wakati tunafika Paris mnamo Juni, tunataka kuona ahadi thabiti na uwekezaji mezani, na harakati imara za wadau mbalimbali kwa ajili ya usawa wa kijinsia. Utambuzi wa haki sawa za nusu ya idadi ya watu wote duniani ni mapigano ya haki za binadamu ambayo haijakamilika ya karne hii."

Kongamano hili la kizazi cha usawa limeandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women kwa msaada mkubwa wa serikali za Mexico na Ufaransa ambako kutafanyika sehemu ya pili ya kongamano hili mwezi juni mwaka huu. 

Pia wadau wengine mbalimbali wamesaidia kuwezesha kongamano hilo.