Skip to main content

Kwa mamilioni ya raia wa Syria maisha ni karaha tupu msaada wa kimataifa wahitajika:UN

Mtoto akiangalia eneo lilofurika kambi ya Kafr Losin Kaskazinimagharibi mwa Syria.
UNICEF/Khaled Akacha
Mtoto akiangalia eneo lilofurika kambi ya Kafr Losin Kaskazinimagharibi mwa Syria.

Kwa mamilioni ya raia wa Syria maisha ni karaha tupu msaada wa kimataifa wahitajika:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza fedha za ufadhili wa mipango ya misaada kwa ajili ya mamilioni ya watu nchini Syria na ukanda mzima, ambao wanategemea msaada wa kuokoa maisha na na kuweza kujikimu baada ya miaka kumi ya vita. 

Pamoja na nyongeza ya athari kubwa za janga la coronavirus, au COVID-19 "hakuna raha kwa raia nchini Syria", Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu wa masuala ya Kibinadamu  na misaada ya dharura (OCHA), shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Maendeleo wa (UNDP) wamesema hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo. 

Kwa mujibu wa Mark Lowcock mkuu wa OCHA “Imekuwa ni miaka kumi ya kukata tamaa na maafa kwa Wasyria. Sasa kuporomoka kwa hali ya maisha, kushuka kwa uchumi na COVID-19 vimesababisha njaa zaidi, utapiamlo na magonjwa”. 

Nchini Syria na katika eneo la ukanda huo, watu milioni 24 wanahitaji msaada wa kibinadamu au aina nyingine ya msaada ikiwa ni milioni 4 zaidi ya mwaka jana na idadi ya juu zaidi tangu mzozo ulipoanza. 

Bwana Lowcok ameongeza kuwa  “Watu wengi wanahitaji msaada zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote wakati wa vita, na watoto lazima warudi kujifunza. Uwekezaji katika ufadhili na ubinadamu daima ni mzuri lakini kudumisha viwango vya msingi vya maisha endelevu kwa watu nchini Syria pia ni kiungo muhimu cha amani endelevu na hiyo ni kwa masilahi ya kila mtu”. 

Milioni 24 wanaohitaji msaada 

Taarifa ya mashirika hayi imetolewa kabla ya mkutano wa tano wa siku mbili wa Brussels wa ahadi ya msaada kwa kwa Syria, ambao umeanza leo tarehe 29 na kuisha kesho 30 Machi, kuhamasisha na kuchangisha fedha ili kusaidia chakula, maji na usafi wa mazingira, huduma za afya, elimu, chanjo ya watoto na makazi ya wakimbizi wa ndani nchini Syria. 

Fedha hizo pia zitasaidia mipango ya msaada wa kugawa pesa taslimu, fursa za ajira na mafunzo, na huduma zingine kama vile kupata elimu ya msingi na sekondari, kwa kushirikiana na mifumo ya kitaifa katika nchi jirani, kulingana. 

Kwa jumla, zaidi ya dola bilioni 10 zinahitajika kusaidia kikamilifu Wasyria na jamii zenye uhitaji zinazopokea na kuhifadhi wakimbizi, yameongeza mashirika hayo .  

Kiasi hicho cha fedha kinajumuisha angalau dola bilioni 4.2 kwa ajili ya kuchukua hatua ndani ya Syria na dola bilioni 5.8 bilioni kwa wakimbizi na jamii za wenyeji katika eneo hilo. 

Kwa sababu ya janga la coronavirus, Mkutano huo wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Syria unafanyika kwa nyia ya mtandao. 

Hatua zilizopigwa ziko hatarini 

Kwa upande wake Filippo Grandi, kamishna mkuu wa shirika la Wakimbizi, UNHCR  ameonya kuwamafanikio makubwa yaliyopigwa na jumuiya ya kimataifa katika mzozo wa Syria kwa miaka mingi tayari yako hatarini. 

“Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuwapa kisogo wakimbizi au wenyeji wao. Wakimbizi na wenyeji wao hawapaswi kupata chochote pungufu kutoka kwetu isipokuwa kujitolea kwetu, mshikamano na msaada. Kushindwa kufanya hivyo itakuwa janga kubwa kwa watu Syria na ukanda mzima”. 

Naye Achim Steiner mkuu wa UNDP, aliendelea kusema kwamba “Athari za janga la COVID-19, juu ya miaka 10 ya mzozo vinawaweka wakimbizi wa Syria na jamii za wenyeji katika kilele cha madhila. Sasa kuliko hapo awali msaada wa jamii ya kimataifa unahitajika zaidi ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya kuokoa maisha na kukabiliana na hali ya dharura ya maendeleo ambayoinaukabili ukanda huo kwa sasa”. 

Katika mkutano wa mwaka jana huko Brussels, wahisani waliahidi ufadhili wa dola bilioni 5.5 kusaidia shughuli za kibinadamu, kujenga mbnepo na shughuli za maendeleo kwa mwaka 2020.