Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani mauaji ya raia wakati wa masako Myanmar

Kijana akiwasha mishumaa mjini Yangon , Myanmar
Unsplash/Zinko Hein
Kijana akiwasha mishumaa mjini Yangon , Myanmar

Guterres alaani mauaji ya raia wakati wa masako Myanmar

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji ya makumi ya raia wakiwemo Watoto na vijana yaliyofanya leo na vikosi vya ulinzi nchini Myanmar.

Katika taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq, Katibu Mkuu António Guterres amesema, "kuendelea kwa msako wa kijeshi hakukubaliki na kunahitaji hatua thabiti, zenye umoja na imara za  kimataifa".

Wakati jeshi la Myanmar liliposherehekea siku ya vikosi vya jeshi na gwaride katika mji mkuu wa nchi hiyo Yangon, wanajeshi na polisi waliwakandamiza waandamanaji katika kile kilichosababisha idadi kubwa zaidi ya watu kufa kwa siku moja tangu maandamano yalipoanza mwezi uliopita.

"Wanajeshi walisherehekea siku ya vikosi vya jeshi kwa kufanya mauaji ya watu wengi dhidi ya watu ambao wanaopaswa kuwatetea", ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Tom Andrews, Mwakilishi maalum kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Myanmar.

Ameongeza kuwa wanarakati wa utiifu wa kiraia wanajibu kwa kutumia "silaha yenye nguvu ya amani na kuutaka ulimwengu kuchukua hatua kwaajili ya watu wa Myanmar.”

Hali inayozidi kudorora

Tarehe Mosi Februari, kufuatia uchaguzi mkuu ambao chama cha Aung San Suu Kyi cha Ligi ya Kitaifa ya Demokrasia kilishinda kwa kishindo, jeshi lilichukua udhibiti wa nchi na kutangaza hali ya hatari ya mwaka mzima.

Wakatiu Bi. Suu Kyi akiendelea kuzuiliwa katika eneo lisilojulikana, waandamanaji wamemiminika mitaani.

Mbali na kuweka amri ya kutotoka nje na vizuizi vingine, vikosi vya usalama vimetumiarisasi za maji, risasi za mpira na risasi za moto kujaribu kutawanya waandamanaji, kulingana na duru za habari.

Suluhisho la haraka linahitajika

"Ni muhimu kupata suluhisho la haraka la mgogoro huu", amesisitiza Katibu Mkuu.

Na pia amerejea ombi la lazima kwa wanajeshi kujiepusha na vurugu na ukandamizaji na akisema kwamba "wale waliohusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa Myanmar lazima wawajibishwe".