Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde Kenya hakikisheni uamuzi wowote kuhusu wakimbizi ni suluhu muafaka na endelevu:UNHCR  

Kakuma, kambi ya wakimbizi  nchini Kenya
UN/Esperanza Tabisha
Kakuma, kambi ya wakimbizi nchini Kenya

Chonde chonde Kenya hakikisheni uamuzi wowote kuhusu wakimbizi ni suluhu muafaka na endelevu:UNHCR  

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeisihi serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba maamuzi yoyote itakayofanya kuhusu kambi za wakimbizi zilizoko nchini humo yanakuwa ni suluhu endelevu kwa wakimbizi hao.

Rai hiyo ya UNHCR iliyotolewa kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumatano jioni imekuja baada ya serikali ya Kenya kutoa taarifa ya kuelezea nia yake ya kutaka kuzifunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma zilizoko nchini humo. 

UNHCR imesema inawashukuru wat una serikali ya Kenya kwa kuwakirimu wakimbizi na waomba hifadhi kwa miongo mingi na kwamba “Inatambua athari zilizoletwa na ukarimu huo kwa Kenya.” 

Kwa mujibu wa UNHCR taarifa waliyopewa na maafisa wa serikali ya Kenya kuhusu nia yake ya kuzifunga kambi za Dadaab na Kakuma ni ya ndani ya muda mfupi na hivyo llimesema “UNHCR inatiwa hofu na athari za uamuzi huu kwa usalama wa wakimbizi nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kwa mazingira ya sasa ya janga la COVID-19. Tutaendelea na mazungumzo na serikali ya Kenya kuhusu suala hili.” 

Wameitaka serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba maamuzi yoyote yanaruhusu kupatikana kwa suluhu muafaka na endelevu na kwamba wale wanaoendelea kuhitaji ulinzi wanaupata. 

Pia shirika hilo limesema liko tayari kuisaidia serikali ya Kenya kusongesha na kuimarisha kazi inayoendelea ya kusaka suluhu ambazo ni za mpangilio, endelevu na zinazoheshimu haki za wakimbizi. 

Kambi ya Dadaab ilianzishwa mwaka 1991 baada ya wimbi kubwa la watu kuvuka mpaka na kuingia Kenya wakikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia na kwa sasa inahifadhi wakimbizi na waomba hifadhi takriban 219,000 na makazi ya wakimbizi ya Kakuma  yaliyogawanyika katika sehemu nne , Kakuma 1, 2 , 3 na 4 yalianzishwa mwaka 1992 kufuatia kuwasili kwa wimbi la wakimbizi kutoka Sudan waliojulikana kama “Lost Boys of Sudan” na baadaye mwaka huohuo waliwasili wakimbizi toka Ethiopia baada ya kuangushwa kwa serikali.  

Makazi hayo yanahifadhi wakimbizi na waomba hifadhi takriban 200,000. 

Serikali ya Kenya kwa ujumla inahifadhi wakimbizi na waomba hifadhi wapatao 500,000 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Somalia, Sudan Kusini, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo DRC, Burundi na Rwanda.