Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkwamo wa kisiasa Somalia unatia wasiwasi: Guterres

Mvulana akiangalia wakati vijana wakicheza soka katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Mogadishu nchini Somalia.
UN Photo/Tobin Jones)
Mvulana akiangalia wakati vijana wakicheza soka katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Mogadishu nchini Somalia.

Mkwamo wa kisiasa Somalia unatia wasiwasi: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amerejea kusema kwamba mkwamo wa kisiasa unaondelea nchini Somalia kuhusu kufanya uchaguzi mkuu licha ya duru kadhaa za majadiliano miongoni mwa wadau wa kisiasa nchini humo katika ngazi zote ni suala linalomtia wasiwasi mkubwa. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Jumanne usiku mjini New York Marekani Katibu Mkuu amesema kuendelea kwa mkwamo huo huo wa kisiasa kwa muda mrefu kuna hatarisha utulivy wa taifa hilo la Pembe ya Afrika na mustakbali wa watu wa Somalia ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu na mazingira tete ya usalama. 

Bwana. Guterres wameitaka serikali ya shirikisho ya Somalia na viongozi wa majimbo ya shirikisho kujihusisha katika mazungumzo na kupanga mkutano wa dharura bila masharti ili kutatua tofauti zao kuhusu mchakato wa uchaguzi na kufikia muafa wa jinsi ya kusonga mbele.

Pia amekaribisha ahadi ya viongozi wa Somalia ya tarehe 17 Septemba kuhusu muundo wa uchaguzi na kuwatolea wito wa kuafiki haraka utekelezaji wake na kufanya uchaguzi bila kuchelewa. 

Katibu Mkuu amerejea kusema kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti kuisaidia Somalia kuelekea amani, utulivu na mafanikio.