Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Alphonso Davies msakata gozi wa Bayern FC  atangazwa kuwa balozi mwema wa UNHCR

Mpira wa mguu
IOM Belarus
Mpira wa mguu

Alphonso Davies msakata gozi wa Bayern FC  atangazwa kuwa balozi mwema wa UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutana na balozi mwema mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, si mwingine bali ni mwana kaandanda nyota Alphonzo Davies, anayesakata gozi kwenye timu ya FC Bayern Munich ya Ujerumani lakini pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Canada. Ametangazwa leo kufuatia mchango wake mkubwa kwa wakimbizi.

Kufuatia kutangazwa huko Davies ambaye asili yale ni Liberia lakini sasa ni raia wa Canada, anakuwa mwanasoka wa kwanza na raia wa kwanza wa Canada kuwa balozi mwema wa UNHCR

Akilipokea jukumu lake jipya la kuwa balozi mwema Davies amesema,“Ninajivunia kujiunga na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, kama Balozi mwema. Uzoefu wangu mwenyewe unanifanya nitake kuwatetea wakimbizi, kusambaza hadithi zao na kusaidia kuleta mabadiliko.” 

Akimkaribisha Davies kwenye timu ya malozi wema wa UNHCR Kamisha mkuu wa shirika hilo Filippo Grandi akafunguka ,“Alphonso Davies anadhihirisha nguvu ya michezo na ni heshima kubwa sana yeye kujiunga nasi. Michezo ina uwezo wa ajabu wa kuleta matumaini, kuponya na kusaidia kujenga mustakbali kwa wale waliolazimika kukimbia. Katika kazi yetu na wakimbizi tunashuhudia kila siku tofauti gani za kuwainua ambazo michezo inaweza kuzifanya katika maisha yao. Hadithi yake binafsi, talanta yake, ushindi kama mcheza soka mahiri na kujitolea kwake kuwasaidia wakimbizi ni vya kuvutia. Ninashauku kubwa ya kufanya kazi naye.” 

Alphonso alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Ghana wakati wazazi wake walipokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia.

Na anasema kambi ya wakimbizi ilitoa hifadhi na usalama kwa familia yake na hajui angekuwa wapi leo endapo UNHCR isingeipelek familia yake nchi ya tatu Canada akiwa na umri wa miaka 5. 

Alipotimiza miaka 15 ndio alipoanza kucheza soka ya kulipwa na alipotimiza miaka 20 alichaguliwa kujiunga na timu ya taifa ya soka ya Canada na kumfanya kuwa mchezaji mdogo kabisa kuwahi kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo. 

Davies amedhamiria kuunga mkono kazi za UNHCR na kutumia nguvu ya michezo kuwasaidia wale waliolazimika kukimbia makwao ili wawe na mustakbali bora, “Nataka watu wajue kuhusu umuhimu wa kuwasaidia wakimbizi popote waliko, makambini, au mijini, katika nchi jirani au katika nchi ya tatu kama vile Canada. Wakimbizi wanahitaji msaada wetu ili kuishi, lakini pia fursa za elimu na michezo ili waweze kufikia uwezo wao na kushamiri.” 

Alphonso alianza kuisaidia UNHCR mwaka  2020, ikiwa ni pamoja na kurusha mashindano ya mojakwa moja ya wakimbizi na Februari mwaka huu 2021 aliisaidia serikali ya Canada kuzindua kampeni iitwayo “Pamoja kwa kujifunza” ya kuchagiza fursa za elimu bora kwa wakimbizi kote duniani.