Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa mpya ya TB kunusuru maisha ya wengi- UNITAID 

Mgonjwa anayepokea tiba dhidi ya kifua kikuu Lima, Peru.
PAHO/Joshua Cogan
Mgonjwa anayepokea tiba dhidi ya kifua kikuu Lima, Peru.

Dawa mpya ya TB kunusuru maisha ya wengi- UNITAID 

Afya

Ikiwa leo ni siku ya ugonjwa wa Kifua au TB  duniani, Umoja wa Mataifa umetangaza Habari njema za tiba dhidi ya gonjwa hilo, tiba ambayo siyo tu kwamba gharama yake ni nafuu, bali pia ni ya muda mfupi na vidonge vinavyotumika ni vichache. 

Kupitia shirika la kimataifa la kufanikisha uwepo wa tiba nafuu duniani, UNITAID linaloratibiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, dawa hiyo mpya ni Rifapentine ambayo tayari imeanza kutolewa katika nchi 5 zenye kiwango kikubwa zaidi cha TB barani Afrika ambazo ni  Ethiopia, Ghana, Kenya, Zimbabwe na Msumbiji. 

Msemaji wa UNITAID Herve Verhoosel akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswsi amesema  “UNITAID ina furaha kuwajulisha kuhusu tiba mpya ya gharama nafuu. Tiba mpya gharama yake ni nafuu kwa asilimia 70 kuliko dawa zaa wali. Inaitwa Rifapentine na kwa majadiliano kati ya UNITAID na wadau wake, dawa hii inaweza kupatikana katika nchi zaidi ya 100 kwa gharama yad ola 15 badala yad ola 45.” 

WHO inapendekeza matumizi ya tiba hii mpya kwa watu wagonjwa wa Kifua Kikuu kilichofikichika ambao wanaishi na virusi vya Ukimwi, VVU na wagonjwa wengine wenye Kifua Kikuu wa umri wowote. Utafiti umebaini kuwa wagonjwa wana uwezo mkubwa wa kukamilisha matibabu katika kipindi kifupi. 

Wagonjwa wa Kifua Kikuu wanaweza kuambukiza ugonjwa huo kwa watu kati ya 10 hadi 15 wanaokaribiana nao kwa mwaka mzima ambapo UNITAID inasema bila tiba sahii, asilimia 45 ya watu wasio na VVU wenye Kifua Kikuu na watu wenye VVU na Kifua Kikuu wanaweza kufariki dunia. 

Ameongeza “licha ya Kifua Kikuu kuwa ugonjwa unaozuilika na kutibika, bado ni moja ya magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza ukisababisha vifo vya watu milioni 1.5 kila mwaka wakiwemo watu 250,000 wanaoishi na virusi vya Ukimwi.” 

Maambukizi ya TB 

Inakadiriwa kuwa mwaka 2019, watu wapatao milioni 10 waliambukizwa Kifua Kikuu, idadi ambayo imekuwa ikipingua taratibu mno katika miaka ya karibuni. Katika idadi hiyo milioni 5.7 ni wanaume, milioni 3.2 wanawake na milioni 1.1 ni watoto na idadi kubwa wanaishi katika nchi za kipato cha chini na kati. 

Kikanda, ukanda wa Kusini-Mashariki mwa Asia una asilimia 44 ya wagonjwa wa Kifua Kikuu,  ukifuatiwa na Afrika asilimia 25 na Pasifiki Magharibi asilimia 18. 

Kitaifa, nchi  zenye wagonjwa zaidi wa Kifua Kikuu ni India, Indonesia, China, Ufilipino, Pakistani, Nigeria, Bangladesh na Afrika Kusini. 

Janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 nalo limekuwa mwiba katika tiba dhidi ya kifua kikuu kwa kuwa linavuruga utoaji wa huduma za Kifua Kikuu. 

UNITAID inasema kuwa vifo kutokana na Kifua Kikuu duniani kote vinaweza kuwa vimeongezeka kutoka 200,000 hadi 400,000 mwaka 2020 iwapo wagonjwa wa Kifua Kikuu hawakuwa wamepatiwa tiba. 

Hata hivyo Bwana Veroosel amesema kutokana na tiba hii mpya, zaidi ya wagonjwa milioni 3 wanaweza kupatiwa tiba hii mwaka huu wa 2021.