UNICEF yatiwa hofu na mustakabali wa watoto kufuatia moto Cox’s Bazar

23 Machi 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema lina hofu kubwa juu ya mustakabali wa watoto wakimbizi wa kabila la Rohingya kufuatia moto mkubwa uliowaka katika kambi yao huko Cox’s Bazar siku ya Jumatatu ya tarehe 22 mwezi huu wa machi ambapo watu wamepoteza maisha na wengine wamejeruhiwa.
 

Msemaji wa UNICEF mjini Geneva, Uswisi James Elder amewaambia waandishi wa habari hii leo, “watendaji wa UNICEF walioko eneo hilo wanasema kiwango cha moto huo ni kikubwa kuwahi kushuhudiwa kwenye kambi hiyo. Wakati juhudi zilifanyika kuudhibiti, moto huo uliendelea kusambaa kwenye kambi na ulipunguza kasi pale tu ulipofika maeneo ya barabara kuu na maji.”

Bwana Elder amesema moto huo umefanya hali kuwa mbayá kwa watoto akisema  “kambi hiyo ina zaidi ya watoto 450,000 wanaohitaji msaada. Ripoti zinaonesha kwamba watoto ni miongoni mwa waliojeruhiwa na kwamba watoto wengine wametengana na familia zao.”

Ameongeza kuwa UNICEF ina vituo kadhaa vya mafunzo kwa watoto kambini humo na wana hofu kuwa idadi kubwa vimeteketezwa kwa moto, idadi ambayo hadi sasa haijathibitishwa.

Hata hivyo amesema hivi sasa wanatathmini mahitaji ya haraka na dharura ya watoto na familia zao, “tumehamasisha vikundi vya kutoa huduma ya afya kuelekeza huduma ya kwanza na pia wafanyakazi wa kujitolea wanahamisha wakimbizi kutoka makazi yao ambayo yameungua kwa moto.”

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa moto huo wa jana Jumatatu umesababisha vifo vya watu 15 huku mamia kadhaa wamejeruhiwa na makumi ya maelfu hawana makazi.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter