Hali ya hewa na maji ni lila na fila havitengamani: Guterres 

23 Machi 2021

Katika kuadhimisha siku ya utabiri wa hali ya hewa duniani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema hali ya hewa na maji havitengamani na kimoja hakiwezi kuwepo bila kingine vivyo hivyo katika maisha ya binadamu.

Guterres ameyasema hayo katika ujumbe wake wa siku hii akiongeza kuwa maji huvukiza mvuke kutoka kwenye uso wa dunia kwenda angani, ambapo hujiingiza kwenye mawingu ambayo husafirishwa kote ulimwenguni na kisha kuleta mvua na theluji ambayo vinarudisha tena maji safi kwenye ardhi ya dunia, mito, maziwa na barafu.  

Na hii ndio inayoendesha maisha kwenye dunia kwa kuwa hali ya hewa husukuma mzunguko wa maji, na kutabiri hali ya hewa ya dunia. 

Ujumbe huo pia umesisitiza kuwa “Mzunguko huu mara nyingi huchukuliwa kuwa ni wa kawaida. Lakini ni kitovu cha malengo yetu mengi ya maendeleo endelevu kuanzia katika kutokomeza njaa, kuhakikisha afya na ustawi, kuwezesha viwanda vyenye tija, kudumisha jamii zinazostawi na kufungua uwezo wa kuwa na nishati nafuu na safi kwa wote.” 

Hata hivyo ameonya kwamba mabadiliko ya tabianchi yanavuruga mzunguko huu na kugawanya uwezo wa upatikanaji wa maji kote duniani. 

“Hii inamaanisha ongezeko la mafuriko kwa wengine na ukame wa muda mrefu kwa wengine, dunia yetu tayari inakabiliwa na changamoto lukuki za maji kuanzia matumizi yasiyo endelevu, hadi nusu ya watu wote duniani kukabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kwa takriban mwezi mmoja kwa mwaka. Wakati mahitaji ya kimataifa ya maji yakiendelea  kuongezeka tunakabiliwa za zahma kubwa ya maji.” Amesema Katibu

Na kuongeza kuwa ndio maana maudhui ya siku ya mwaka huu ni yanajikita katika hali ya hewa na maji.  

“Tunahitaji kudhibiti hali ya hewa na maji katika njia iliyoratibiwa na endelevu ili kushughulikia usambazaji wa maji na changamoto za maji mengi kupita kiasi, machache kupita kiasi au yaliyochafuliwa kupindukia. Hatuwezi kusimamia kile ambacho hatupimi. Uboreshaji wa ufuatiliaji na utabiri wa hali ya hewa ni muhimu ili kuunga mkono sera madhubuti za usimamizi wa maji na huduma za utoaji wa taarifa za mapema kuhusu mafuriko na ukame. “ 

 Kwa mantiki hiyo katika siku hii Guterres ameitaka dunia kuthamini uhusiano uliopo baina ya hali ya hew ana maji na umuhimu wa mzunguko wa maji. 

Ametaka pia kuongezwa juhudi za kuzisaidia jamii za hali ya hewa na maji ili kuendeleza usimamizi mzuri wa vyanzo vya maji.  

Akihitimisha ujumbe wake  amesema “Hebu na tuhesabu kila tone la maji, kwa sababu kila tone lina umuhimu. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter