Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa wanawake kwenye vikosi kazi dhidi ya COVID-19 haukubaliki

Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda
© UNICEF
Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda

Ukosefu wa wanawake kwenye vikosi kazi dhidi ya COVID-19 haukubaliki

Wanawake

 Idadi ya wanaume kwenye vikosi kazi vya kitaifa vya kupambana na ugonjwa wa Corona au COVID-19 duniani kote ni kubwa kuliko wanawake, zimeonesha takwimu mpya zilizotolewa leo na Umoja wa Mataifa na wadau wake.
 

Utafiti huo kutoka shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP na Chuo Kikuu cha Pittsburgh umesema katika vikosi kazi hivyo katika watu wanne, wanaume ni watatu na mwanamke ni mmoja.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo New York, Marekani na UNDP na wadau wake, ukosefu huo wa uwiano kwenye vikosi kazi hivyo utakwamisha harakati za kukwamua wanawake kutoka katika janga la COVID-19.

“Dunia inapotimiza mwaka mmoja tangu kuibuka kwa COVID-19, kwa wastani wanawake ni asilimia 24 tu ya wanachama kwenye vikosi kazi 225 vya kukabiliana na COVID-19 kwenye nchi 137. Na katika vikosi kazi 26 hakuna kabisa wanawake,” zimeonesha takwimu hizo.

Wanawake wanaengulia kimfumo

hizi mpya zinakuja wakati dunia inaendelea kusaka mbinu za kukabiliana na janga la Corona na athari zake kwa wanawake; kuanzia jukumu lao kama whudumu wa afya kwenye mstari wa mbele, huku wakipoteza ajira zao kutokana na kudorora kwa uchumi hadi kuongezeka kwa ukatili wa majumbani na mzigo wa malezi usio na ujira wowote vyote vikitishia kutumbukiza wanawake wengine milioni 47 kwenye lindi la umaskini..

Mtawala Mkuu wa UNDP Achim Steiner akizungumzia ripoti hiyo amesema, “wanawake wamekuwa mstari wa mbele kwenye harakati dhidi ya COVID-19 ,wakichangia asilimia 70 ya wahudumu wa afya duniani kote. Hata hivyo wameenguliwa kimfumo kutoka kwenye michakato ya kupitisha uamuzi wa jinsi ya kushughulikia madhara ya janga la Corona. Takwimu hizi za kufungua macho, mathalani, zinaonesha ni nchi 8 pekee duniani kote ndio zina uwiano sawa wa idadi ya wanawake na wanaume katika vikosi kazi vya kukabiliana na Corona.”

Amesisitiza kuwa ushiriki jumuishi na kamilifu wa wanawake kwenye taasisi za umma ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mahitaij yao yanazingatiwa wakati wa maamuzi ya msingi, na kwamba maamuzi ya sasa ni muhimu kwa mustakabali wa vizazi vijavyo.

Bila wanawake hatua zinazochukuliwa hazitafanikiwa

Amekumbusha kuwa, “bila wanawake kwenye dhima za kupitisha uamuzi, hatua dhidi ya COVID-19 ziko katika nafasi kubwa za kutokuwa na maslahi kwa wanawake na zinaweza kuchochea fursa zisizo sawia za kujikwamua kutoka kwenye janga na kurejesha nyuma maendeleo yaliyofikiwa katika miongo kadhaa iliyopita.
Ni kwa mantiki hiyo, UNDP na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-Women wanasihi serikali kuhakikisha wanawake, siyo tu wana ushiriki sawa kwenye harakati za kujikwamua kutoka madhra ya janga la Corona bali pia wana fursa sawa za maamuzi.

Bwana Steiner amesema ili hatua dhidi ya COVID-19 ziwe fanisi, sera na mipango yoyote ile lazima iwe na mtazamo wa kijinsia lakini hadi sasa nchi 32 hazina kabisa mikakati rafiki ya kijinsia katika kukabiliana na madhara ya janga la sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaj iwa UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema ni jambo lisilofikirika ya kwamba “tunaweza kushughulikia janga la kibaguzi zaidi kuwahi kukumbana nalo, bila ushiriki kamilifu wa wanawake. Hivi sasa wanaume wamejipatia jukumu lisilowezekana la kupitisha uamuzi sahihi kuhusu wanawake bila kunufaika na mtazamo wa wanawake kwenye suala hilo. Hili linapaswa kushughulikiwa haraka ili tufanye kazi pamoja kwa ajili ya mustakabali ambao una usawa, wenye mtazamo wa kijinsia na wa manufaa.”