Ubaguzi wa rangi upo, ubaguzi wa rangi unaua, sasa ni wakati wa kuutokomeza:Guterres

19 Machi 2021

 Ubaguzi wa rangi kwa bahati mbaya sana upon a unaendelea katika nchi zote na katika jamii zote duniani na mizizi yake imekita kutokana na karne na karne za ukoloni na utumwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika tukio la kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi iliyofanyika leo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, asilimia kubwa ikiwa ni kwa njia ya mtandao.
Bwana. Guterres amesema “Tunauona ubaguzi ulioenea na kutengwa na kuteswa kwa watu wa asili ya Kiafrika. Tunauona katika dhuluma na ukandamizaji unaovumiliwa na watu wa kiasili na makabila mengine madogo. Tunauona katika maoni yenye kuchukiza ya wanaoona wazungu ni bora zaidi na kwenye vikundi vingine vyenye msimamo mkali. Tunaona pia ubaguzi wa rangi na ubaguzi katika chuki dhidi ya Uyahudi, chuki dhidi ya Waislamu, unyanyasaji wa jamii ndogo za Kikristo na aina zingine za kutovumiliana na chuki dhidi ya wageni. Na tumeuona ubaguzi wa rangi katika vurugu za hivi karibuni za kuchukiza dhidi ya watu wa asili ya Asia, wanaolaumiwa bila haki kwa kusambaza COVID-19.”
 Ameongeza kuwa ubaguzi upon a unaendelea kuwepo kwani unashuhudiwa pia katika upendeleo uliojengeka katika kutambua sura na akili bandia.

Kumbukumbu ya kifo cha George Floyd aliyeuawa na polisi
Hazel Plunkett
Kumbukumbu ya kifo cha George Floyd aliyeuawa na polisi

Hatua za kupinga ubaguzi

Katika ujumbe wake kwa ajili ya siku ya kupinga ubaguzi wa rangi , Katibu Mkuu António Guterres amesisitiza kwamba “ubaguzi lazima ulaaniwe bila kujizuia, bila kusita na bila kikomo. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ametaka kukomeshwa kwa vitendo vya polisi kukwepa skutokana na vurugu wanazozifanya na hilo litajadiliwa na mkutano wa viongozi wa ulimwengu baadaye mwezi Septemba.”
Jumapili hii, Machi 21, Umoja wa Mataifa unaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi na kaulimbiu ni "Vijana kusimama dhidi ya ubaguzi wa rangi".
Katika ujumbe huo pia António Guterres amekumbuka jinsi, mwaka jana, watu kote ulimwenguni walivyomiminika mitaani kupinga "janga baya la ulimwengu la ubaguzi wa rangi."

Haki za binadamu

Waandamanaji wakishiriki kupinga mauaji ya watu weusi nchini Uingereza
Unsplash/Arthur Edelmans
Waandamanaji wakishiriki kupinga mauaji ya watu weusi nchini Uingereza

Nako mjini Geneva Uswisi hii leo , Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Michelle Bachelet, ametoa sahihisho la Azimio namba 43/1, ambalo linatoa wito wa kutathminiwa kwa ubaguzi wa kimfumo na ukiukaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na wa vyombo vya iusalama dhidi ya watu wenye asili ya  Kiafrika.
Wiki iliyopita, alikutana na wanafamilia kadhaa wa kizazi chenye asili ya Kiafrika  waliouawa na maafisa wa polisi.
Bachelet amesema "ameguswa sana maelezo waliyompya ya kiwewe kinachoendelea cha kupoteza mtoto au kaka kwa njia ya ghafla na ya vurugu.
Kamishna mkuu aamesema kwamba miezi 10 baada ya kuuawa kwa George Floyd huko Marekani kesi hiyo itahukumiwa, lakini sivyo katika sehemu zingine za za dunia na kwa familia nyingi ambazo hazioni haki ikitendeka.
Bachelet ameongeza kuwa "kutokujali uhalifu ambao huenda ulifanywa na maajenti wa serikali kunaumiza sana maadili ya msingi na mshikamano wa kijamii wa kila taifa. "
Kwake, "hakuna polisi au wakala yeyote wa kampuni yoyote ya serikali anayepaswa kuwa juu ya sheria. kwa sababu hii ni kanuni ya msingi ya sheria."
Kamishna mkuu pia alifahamisha kuwa atawasilisha ripoti kwa Baraza la Haki za binadamu HRC juu ya mada hiyo mnamo Juni, na idadi ya mapendekezo ya kumaliza ubaguzi wa kimfumo na unyanyasaji wa polisi dhidi ya Waafrika na watu wenye asili ya Afrika na kuwasaidia wahanga.

Kuhusu siku hii

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN News/Daniel Johnson
Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

Machi 21 ilichaguliwa kuwa siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi kwa sababu mnamo 1960, polisi huko mjini Sharpeville, Afrika Kusini, walifyatua risasi na kuua watu 69 waliokuwa wakifanya maandamano ya amani dhidi ya kupitishwa kwa sheria za serikali ya ubaguzi wa rangi.
Mwaka 1979, Baraza Kuu liliidhinisha mpango wa shughuli kwa nusu ya pili ya Muongo wa hatua ya kupambana na ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa kutenga watu.
Wakati huo, iliamuliwa kuwa nchi zote wanachama zingeandaa wiki ya ya matukio mbalimbali kuhusu mada hiyo.
Mwezi Septemba mwaka huu, Baraza Kuu litawakutanisha viongozi wa wa dunia mjini New York Marekani kuadhimisha miaka 20 ya Azimio la Durban na programu yake ya utekelezaji.
Mkutano huo utakuwa na kaulimbiu "Fidia, haki ya rangi na usawa kwa watu wa asili ya Kiafrika."
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter