Skip to main content

UNHCR na wadau wa misaada wazindua ombi la dola bilioni 1.2 kusaidi wakimbizi wa Sudan Kusini

Mwanamke akiwa Dorein, Sudan Kusini, akiwa ameketi kandoni mwa mgao wa chakula uliotolewa na WFP kwa ajili ya familia yake.
WFP/George Fominyen
Mwanamke akiwa Dorein, Sudan Kusini, akiwa ameketi kandoni mwa mgao wa chakula uliotolewa na WFP kwa ajili ya familia yake.

UNHCR na wadau wa misaada wazindua ombi la dola bilioni 1.2 kusaidi wakimbizi wa Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, na wadau wake wa misaada wamezindua ombi la dola za Marekani bilioni 1.2 kwa ajili ya msaada muhimu wa kibinadamu kwa zaidi ya wakimbizi milioni 2.2 wa Sudan Kusini, theluthi mbili wakiwa ni watoto.

Wakati baadhi ya maendeleo yamefanyika katika kutekeleza makubaliano ya hivi karibuni ya amani, mahitaji ya kibinadamu na ulinzi yamebaki kwa hali ya wakimbizi barani Afrika. Sudan Kusini imekuwa taifa changa kabisa duniani takribani muongo mmoja uliopita lakini leo mamilioni ya watu wake wamefurushwa ama ndani au nje ya mipaka ya nchi hiyo. Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumzia ombi la ufadhili anasema,"Leo tunazungumzia wakimbizi milioni 2.2 wa Sudan Kusini katika nchi jirani. Na kundi kubwa la wakimbizi hawa ni watoto. Tunazungumzia kuhusu watoto milioni 1.4 wa Sudan Kusini kuwa wakimbizi. Kiasi cha fedha ambacho tumeomba kitawasaidia wakimbizi katika nchi tano jirani lakini pia jamii za wenyeji ambazo zimekuwa zikiwahudumia kwa ukarimu sana."

Janga la COVID-19 pamoja na changamoto zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na mafuriko makali, ukame na nzige wa jangwani zimeifanya hali ambayo tayari ilikuwa mbaya, kuwa mbaya zaidi. Babar Baloch anaeleza,"COVID-19 sio tu janga la kiafya. Ni janga la Maisha pia. Kwa hiyo, pamoja na mahitaji ya maisha kutoweka, tunaona mgao wa chakula, wakimbizi na jamii za wenyeji kutokuwa na chakula cha kutosha, na hatupati fedha za kutosha. Kama mashirika ya kibinadamu inamaanisha hatuwezi kufanya mengi kwa wakimbizi na jamii wenyeji wao. Mahitaji ni makubwa, kuanzia afya, makazi, chakula, maji na usafi wa mazingira, na yanahitaji msaada wa ulimwengu haraka iwezekanavyo."

Wakimbizi wengi wa Sudan Kusini wanaishi katika maeneo ya ndanindani na duni. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda zinaendelea, kwa ukarimu, kuwa wenyeji wa wakimbizi wa Sudan Kusini na kuchukua hatua kuelekea kuwaingiza katika mifumo ya kitaifa  ikiwemo afya na elimu, hali inayoendana sambamba na Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi.