UN yahimiza uwajibikaji kwa watu wanaounga mkono wanamgambo huko Jonglei Sudan Kusini. 

15 Machi 2021

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti leo ukiitaka mamlaka nchini Sudan Kusini kuwawajibisha wanajeshi na viongozi wa kisiasa ambao wanaunga mkono makundi ya jamii yaliyojihami katika eneo la Jonglei ili kuzuia ukatili zaidi.   

Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, makundi ya kijamii yaliyojihami kutoka makabila ya Dinka, Nuer na Murle yalitekeleza mashambulizi ya pamoja katika vijiji Jonglei na Pibor kati ya Januari na Agosti 2020.   

Kamishna Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu Michelle Bachelet amesema, “hatari ya kwamba makundi haya yaliyojihami yataibua ukatili ni kubwa sana kuipuuza. Ni muhimu kwamba serikali ichukue hatua zenye ufanisi kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama vinazuiwa kutokana na kusambaza silaha kutoka kwa hifadhi ya serikali hadi kwa makundi hayo.”   

Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa Serikali ya Sudan Kusini inahitaji kuchukua jukumu kamili kwa madhara yanayowasibu raia wengi. Zaidi ya watu 738 waliuawa na 320 walijeruhiwa, wakati wanawake na watoto wasiopungua 686 walitekwa nyara, na wanawake 39 walibakwa katika kipindi cha miezi nane kilichoangaziwa na ripoti hiyo. Zaidi, makumi ya maelfu walihama makazi yao, mali za raia na vituo vya misaada ya kibinadamu viliporwa na au kuharibiwa, na takribani ng'ombe 86,000 wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 35 ziliibiwa. 

 “Wakati mazungumzo ya amani kati ya jamii zilizoathiriwa yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa, hakuna hatua ya maana imechukuliwa na mamlaka kuchunguza na kushtaki wale waliohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu.” Imesema taarifa. 

Ripoti imeeleza kuwa takribani machifu 50 wa jadi na viongozi wa kiroho, pamoja na viongozi wa kijeshi na kisiasa, waliunga mkono moja kwa moja au kwa namna fulani, mashambulizi yaliyoongozwa na wanamgambo wa jamii huko Jonglei. Na kwamba baadhi ya watu wa Serikali na vikosi vya upinzani walishiriki kikamilifu katika mapigano kulingana na uhusiano wao, au kama sehemu ya hatua iliyohesabiwa ya kuimarisha miungano ya kisiasa, ikionesha changamoto ya kuanzisha jeshi lililounganishwa kikamilifu katika muktadha wa hali ya mgawanyiko wa Sudan Kusini. 

Wakati mamlaka inasema wamechukua hatua kadhaa kushughulikia vurugu hizo, ripoti hiyo inaitaka Serikali kukamilisha uteuzi wa viongozi wa chini kote Jonglei na GPAA, kuchunguza madai yote ya ukiukaji wa haki za binadamu, na kuwashtaki wale waliohusika. Silaha zinazomilikiwa na serikali zinapaswa kuwekwa katika vituo salama vya kuzihifadhi ili kuzuia wizi na kuhakikisha wanachama wa vikosi vya usalama hawawezi kuzipeleka kwa wanamgambo. Hatua za haraka na kali zinapaswa pia kuchukuliwa kuwezesha kutolewa na kuungana tena kwa wanawake na watoto waliotekwa nyara na familia zao. 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter