Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka miwili baada ya kimbunga Idai, Msumbiji bado inahitaji msaada – Guterres 

Mwonekano kutoka kwenye jengo la meya ukionesha uharibifu uliosababishwa na Kimbunga Idai mjini Beira, Msumbiji. (25 Juni 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mwonekano kutoka kwenye jengo la meya ukionesha uharibifu uliosababishwa na Kimbunga Idai mjini Beira, Msumbiji. (25 Juni 2019)

Miaka miwili baada ya kimbunga Idai, Msumbiji bado inahitaji msaada – Guterres 

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe alioutoa mwishoni mwa wiki hii kwa njia ya video, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Msumbiji kwani miaka miwili baada ya kimbunga Idai, bado watu wa nchi hiyo barani Afrika wanahitaji usaidizi. 

Hotuba hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyoitoa kwa lugha ya Kireno na Kiingereza, imekuja siku chache kabla ya Jumatatu ya tarehe 15 Machi, ambapo ni maadhimisho ya pili tangu kimbunga Idai kilipoipiga Msumbiji na kuwaathiri takribani watu milioni 1.8 na kusababisha zaidi ya vifo 600.  

Aidha Bwana Guterres amerudia kueleza kuwa Umoja wa Mataifa unashikamana na watu wa Msumbiji na serikali yao.  

Picha iliyopigwa kutoka angani ikionesha maeneo yaliyoharibiwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.
UN Mozambique
Picha iliyopigwa kutoka angani ikionesha maeneo yaliyoharibiwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji.

 

Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi na msaada kwa mpango wa  msaada wa kibandamu akieleza kuwa familia nyingi Msumbiji bado zinahangaika kuyajenga upya maisha yao kwani  wakati walikuwa katika harakati za kurejea katika hali yao, walipigwa tena na kimbunga Chalane mwezi Desemba na wiki chache baadaye wakapigwa na kimbunga Eloise mnamo mwezi Januari. 

“Nchi hii inahitaji dola milioni 254 kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka.” Ameeleza Guterres. 

Sitasahau nilichokiona 

Pia Guterres amekumbuka uharibifu aliouona wakati wa ziara yake Msumbiji baada ya kupita vimbunga Idai na Kenneth akisema, “sitasahau kile nilichokiona. Niliguswa sana na nguvu na mnepo wa wale wote walioathiriwa na pia nikavutiwa na ushujaa wa timu za misaada ya dharura.” 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akitembelea darasa za shule ya June 25 mji wa Beira nchini Msumbiji, shule ambayo iliharibwa na kimbunga Idai.
UN Mozambique
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akitembelea darasa za shule ya June 25 mji wa Beira nchini Msumbiji, shule ambayo iliharibwa na kimbunga Idai.

 

Vilevile Guterres amesema, "dhoruba za kitropiki zinazidi kuwa kali na za mara kwa mara na inaonesha uzito wa hali hiyo barani Afrika. Kuna maeneo ya bara hilo la Afrika ambayo yana joto kwa kiwango cha mara mbili ya wastani wa ulimwengu.” 

Kisha akaongeza kuwa, “Bara la Afrika ni moja ya maeneo ambayo yana mchango mdogo katika kusababisha mabadiliko ya tabianchi lakini ni moja ya maeneo yanayoteseka zaidi. Kuna haja ya dharura ya kuchukua hatua za haraka kupunguza joto duniani na, wakati huo huo, kuunga mkono mataifa ambayo yako mstari wa mbele katika mabadiliko ya tabianchi ili mnepo wao na uwezo wa kuendana na hali viimarishwe marishwe." 

Mwisho, Bwana Guterres ametoa wito kuwa siku ya kukumbuka kimbunga Idai itumike kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watu wa Msumbiji.