Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa FAO na JR Farms Rwanda kuibua ajira za kilimo zenye utu kwa vijana 

Kilimo ni mkombozi kwa wengi ambao wanajikita na kuzingatia masharti ya wataalamu wa kilimo
FAO/Giuseppe Bizzarri
Kilimo ni mkombozi kwa wengi ambao wanajikita na kuzingatia masharti ya wataalamu wa kilimo

Ubia wa FAO na JR Farms Rwanda kuibua ajira za kilimo zenye utu kwa vijana 

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Rwanda shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limetia saini na kampuni ya kilimo ya JR Farms kwa lengo la kusongesha ushiriki wa vijana kwenye kilimo na kujenga fursa za ajira zenye utu.

JR Farms ni kampuni ya Kinyarwanda inayoendesha shughuli zake nchini humo, halikadhalika Nigeria na Zambia ikijikita katika masuala ya usindikaji wa mazao, uuzaji rejareja wa mazao na kutoa ushauri wa masuala ya kilimo. Lengo la kampuni iyo ni kuhakikina kuna uhakika wa upatikanaji wa chakula, kutokomeza njaa Afrika na kuweka fursa za ajira zenye utu kwa wanawake na vijana barani Afrika.

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo jijini Kigali nchini Rwanda, na Roma Italia,  imesema shirika hilo na JR Farms wameunganisha nguvu kwa lengo la kuendeleza kampuni za masuala ya kilimo zinazoongozwa na vijana kwa kuzipatia fedha kupitia mfuko wa JR Farms wa kilimo kinachojali mazingra, GAF.

Wakulima wajasiriamali hao vijana watapatiwa pia mafunzo na kujengewa uwezo ambao utawapatia fursa ya kupanua wito wao wa mtandao na kukutana na vijana wengine wakulima wajasiriamali.

“Huu ni ubia muhimu na JR Farms, utafungua fursa mpya kwa vijana kwenye sekta ya kilimo na kilimo cha kibiashara na hivyo kujenga fursa za ajira, kuboresha hali ya maisha na kuinua kiwango cha upatikanaji wa chakula,” amesema Gualbert Gbehounou, mwakilishi wa FAO nchini Rwanda.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa JR Farms, Rotimi Opeyemi Olawale amesema kampuni yao itakuwa na dhima muhimu ya kujenga fursa za ajira kwa vijana na kwamba “mpango wetu na FAO siyo tu unatoa fedha bali una usaidizi wa kipekee hasa kwa vijana kwenye kuwajengea uwezo, mafunzo na kuwakutanisha na wajasiriamali wengine kwenye sekta ya kilimo walio na mafanikio.”

Kuwekeza kwa vijana

Ubia wa JR Farms na FAO ni matokeo ya mkutano wa kikanda wa Afrika wa ajira kwa vijana ulioandaliwa na FAO na kufanyika Kigali, Rwanda mwaka 2018 kwa ushirikiano wa Muungano wa Afrika na serikali ya Rwanda.

Ubia huo uko sambamba pia na mkakati mpya wa FAO wa ushirikishaji wa sekta binafsi mwaka 2021-2021 na kupitishwa na Baraza la FAO mwezi Desemba mwaka 2020.

Ubia huu pia unachangia katika miradi mipana zaidi ya FAO huko Guatemala, Ghana, Kenya, Senegal, Rwanda na Uganda na husaidia nchi kupitisha sera zinazojumuisha vijana katika kuendeleza mifumo ya kilimo na chakula.