Uhaba wa maji waweka njia panda maisha ya mamilioni ya watu na mifugo Somalia:OCHA 

12 Machi 2021

Maelfu ya watu nchini Somalia wamelazimika kukimbia makwao tangu mwezi Novemba mwaka jana kwa sababu ya uhaba mkubwa wa maji huku utabiri wa sasa ukionesha kwamba msimu wa mvua unaoanza Machi hadi Juni hautakuwa na mvua za kutosha, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya binadamu na misaada ya dharura OCHA .

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao hii leo mjini Geneva Uswisi msemaji wa OCHA Jens Laerke amesema hali ya ukame tayari imesharipotiwa katika baadhi ya majimbo ya Somaliland, Puntland, Hirshabelle, Galmudug na Jubaland kufuatoa msimu duni wa mvua mwaka jana. 

Ameongeza kuwa “Wasomali wanaokadiriwa kuwa milioni 2.7 wakiwemo Watoto 840,000 wa umri wa chini ya miaka 5 watakabiliwa na mgogoro wa kutokuwa na uhakika wa chakula kati ya mwezi Aprili na Juni. Hilo ni ongezeko la la zaidi ya asilimia 65 ikilinganishwa na viwango vya sasa. Uhaba wa maji pia utaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa.” 

Pia amesema kukosekama kwa mvua kumesababisha kukosekana kwa malisho nah ii inatishia mustakbali wa mifugo Somalia ambayo ni msingi wa maisha ya watu wengi nchini humo. 

Watu waliotawanywa na uhaba huo wa maji wameiambia Ocha kwamba wanahama kwasababu ya kwenda kusaka maji na malisho ya mifugo yao. 

OCHA inasema mashirika ya kibinadamu "kwa sasa yanawafikishia maji watu 300,000 katika maeneo yaliyoathirika na uhaba huo na dola milioni 13 zimetolewa na mfuko wa masuala ya kibinadamu wa Somalia ili kusongesha juhudi za msaada. "

Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF umetenda dola milioni 7 ambazo zitawasili Somaliua punde na dola zingine hadi milioni 20 zitafuatia ili kufadhili hatua za kukabiliana na hali hiyo Somalia. 

OCHA imesema Somalia imekuwa ikikabiliwa na mjanga mbalimbali kwa miongo sasa ikiwemo vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 30, changamoto ya uhakika wa chakula na majanga yatokanayo na hali ya hewa. 

Kwa mwaka huu Umoja wa Mataifa na washirika wake wanalenga kuwafikia watu milioni 4 na misaada ya kibinadamu. 

Na ili kufanikisha hilo OCHA inahitaji dola bilioni 1 na hadi kufikia sasa fedha zilizopatikana ni asilimia 2.5 pekee ya fedha zinazohitajika. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter