Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yazindua kampeni yake ya ‘Ni Kwa Pamoja Tu’

Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX  umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.
© UNICEF/Ahmed Salim Yeslam
Ushirikiano wa kimataifa kupitia mkakati wa COVAX umewezesha chanjo kufika SUDAN na pichani mhudumu wa afya akionesha alama ya ushindi baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya CORONA.

UN yazindua kampeni yake ya ‘Ni Kwa Pamoja Tu’

Afya

Umoja wa Mataifa leo umezindua kampeni ya uchechemuzi kwa umma, ikipatiwa jina Ni Kwa Pamoja Tu, yenye lengo la kutoa wito ili chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 zipatikane kwa wote na popote pale duniani.

Akizundua kampeni hiyo kupitia video maalum hii leo jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mwaka mmoja wa janga la Corona umesababisha wimbi la machungu."Virusi vimeua zaidi ya watu milioni 2.5 na kuacha mamilioni na madhara ya muda mrefu ya kiafya. Familia na uchumi vinaserereka. Hivi sasa na ahadi hii ya chanjo, tunaona nuru kwenye mwanga," amesema Guterres.
Amesema wanasayansi wamefanya maajabu, wametengeneza chanjo salama na thabiti katika muda ambao haujawahi kushuhudiwa, "sasa tuna mbinu ya kukomesha mwenendo wa COVID-19. Lakini ni nchi chache sana ndio zimepata idadi kubwa ya chanjo."

Kampeni inasisitiza umuhimu wa uratibu wa hatua za pamoja za kimataifa ili chanjo zifikia kila nchi kuanzia wahudumu wa afya hadi walio hatarini zaidi.

Guterres amesema chanjo za COVID-19 lazima zionekane kuwa ni bidhaa ya umma duniani kote na kwamba hakuna nchi inaweza kukabili janga la sasa peke yake.

Amesema serikali na sekta za biashara lazima zigawane dozi za chanjo na teknolojia ili usambazaji wa chanjo uwe haraka,.

Guterres amesema COVAX ambao ni mkakati wa chanjo ndio njia bora zaidi ya kufanikisha uwiano sawa wa kupata chanjo kwa kila mtu duniani, hivyo uwezeshwe. Ni kwa mantiki hiyo anasema, "Ni kwa pamoja tu tunaweza kulinda wahudumu wa afya na watu walio hatarini zaidi duniani. Ni kwa pamoja tu tunaweza kukwamua uchumi wetu. Ni kwa pamoja tu tunaweza kumaliza janga hili na kukwamuka. Na ndipo pamoja tunaweza kurejea tena katika vitu vyetu ambavyo tunavipenda."

Akizungumzia kampeni hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema "kwa mwaka mmoja sasa sote tumeshindwa kufanya vile tunavyopenda na wengine, mfano kula pamoja, kukumbatiana, kwenda shuleni na hata kazini. Mamilioni kati yetu tumepoteza mpendwa au maisha yamesambaratika. Ni kwa pamoja tu tunaweza kumaliza janga hili na kubadili zama mpya ya matumaini."

Naye Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa, DGC, Melissa Fleming amesema iwapo wanasayansi duniani waliweza kuanda chanjo hiyo salama na thabiti katika kipindi cha miezi 7, lengo la viongozi duniani sasa nalo livunje rekodi "kwa kutoa fedha za kutosha na kuhamasisha utengenezaji ili kila mtu duniani aweze kupatiwa chanjo."

TAGS: COVID-19, Ni Kwa Pamoja Tu, Only Together