Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliobeba ujauzito bila kutarajia wakati wa janga la COVID-19 waelezea wanayopitia

Takribani wanawake milioni 12 duniain kote wamekumbwa na kuvurugwa kwa huduma za uzazi wa mpango kutokana na janga la COVID-19
© UNFPA/Ollivier Girard
Takribani wanawake milioni 12 duniain kote wamekumbwa na kuvurugwa kwa huduma za uzazi wa mpango kutokana na janga la COVID-19

Waliobeba ujauzito bila kutarajia wakati wa janga la COVID-19 waelezea wanayopitia

Afya

Takribani wanawake milioni 12 wamekumbwa na kuvurugwa kwa huduma zao za afya ya uzazi kutokana na janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19, hali iliyosababisha kuwepo kwa mimba milioni 1.4 zisizopangwa, imesema taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Kathmandu Nepal na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani, UNFPA.
 

Makadirio mapya yaliyotolewa leo yanafuatia takwimu za UNFPA na shirika la Avenir Health.

Makadirio hayo yanazingitaia takwimu halisi za ufuatiliaji ulimwenguni na zimetangazwa hii leo ikiwa imetimia mwaka mmoja tangu COVID-19 itangazwe kuwa ni janga duniani.

Takwimu hizi zinatolewa hata wakati huu ambapo nchi nyingi, hususan za kipato cha juu zinaonesha dalili ya kupungua kwa viwango vya uzazi, ripoti ikisema, “matokeo haya yanaonesha jinsi gani matakwa ya wanawake kuhusu afya ya uzazi yamebadilishwa au kukandamizwa na janga la Corona.”

Makadirio hayo ya UNFPA yametazama kuvurugwa kwa huduma za uzazi wa mpango katika nchi 115 za kipato cha chini na kati katika kipindi husika cha mwaka mmoja.

Huduma hizo zilivurugika kutokana na vizuizi vya kutembea, kuvurugika kwa utaratibu wa usambazaji wa huduma hizo, kumalizika kwa vifaa na huduma za afya kuzidiwa uwezo, na matokeo yake yamekuwa ya kubadili maisha kwa kiasi kikubwa kwa wanawake.

Waliopata ujauzito katikati ya janga la COVID-19

Miongoni mwa wanawake walioshuhudia maisha yao kubadilika kabisa ni Maya Bohara mwenye umri wa miaka 32 kutoka Nepal. Yeye amekuwa akitegemea huduma ya sindano kama njia ya kupanga uzazi kwa miaka 9.

Aliolewa akiwa na umri wa miaka  17, na alijaliwa kupata watoto 4 wakati alipokuwa na umri wa miaka 24. Yeye na mumewe ambaye ni kibarua walitambua hawahitaji tena mtoto mwingine.

Hata hivyo alipotembelea kituo cha afya kwa ajili ya kupata sindano ya mpango wa uzaiz mwezi Juni mwaka jana, “kituo hakikuwa na huduma za uzazi wa mpango wakati huo. Nilikuwa nina hofu mara kwa mara kuwa ninaweza kupata ujauzito ambao sijapanga.”amesema Maya alipohojiwa na UNFPA.

Muda si mrefu baada ya kukosa sindano ya kupanga uzazi, Maya aligundua kuwa  yu mjamzito na alijifungua mwanae tarehe 25 mwezi uliopita wa Februari.

Nilijulishwa kuwa  hakuna. Ingawa mimi na mume wangu tulishaamua kuwa hatutaki tena mtoto, nilipata ujauzito kwa mara ya tatu- Hira Lawad, mkazi wa Nepal

Hira Lawad, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 30, alitembelea kituo hicho cha afya kama Maya mwezi Julai ili kupata huduma za uzazi wa mpango. “Nilijulishwa kuwa  hakuna. Ingawa mimi na mume wangu tulishaamua kuwa hatutaki tena mtoto, nilipata ujauzito kwa mara ya tatu.”

Mimba hizi zisizotarajiwa zimeongeza shinikizo katika familia ambazo tayari zinahaha wakati huu wa janga la Corona kukabili mzigo wa ukosefu wa fedha.

Ingawa Maya alieleza mapema tu kuwa mwanae mchanga anapendwa na familia yake, bado alikiri kuwa mazingira ya malezi hivi sasa ni magumu kuliko ilivyokuwa awali kwa watoto waliotangulia.

“Na kipato hiki kidogo, kulea mtoto wetu wa 5 itakuwa vigumu kwangu mimi na mume wangu,” anasema Maya.

Na madhara ya kulea mimba isiyotarajiwa siyo tu ya kiuchumi, bali inahusishwa pia na ongezeko la vifo vya wajawazito halikadhalika ongezeko la utoaji mimba kwa njia zisizo salama.

Makadirio ya UNFPA yanaonesha kuwa huduma za uzazi wa mpango zilivurugwa zaidi mwezi Aprili na Mei mwaka jana.

Makadirio ya awali ya mwezi Aprili mwaka jana, yalionesha kuwa kuvurugwa kwa kiasi kikubwa kwa huduma za uzazi wa mpango kwa miezi 6 kunaweza kuathiri wanawake milioni 47 katika nchi za kipato cha chini na kati na kusababisha mimba milioni 7 zisizotarajiwa.

Hatua zilizochukuliwa

UNFPA inasema hatua za haraka zilisaidia kupunguza tatizo kwa kurejesha huduma muhimu ikiwemo zile za uzazi wa mpango. Mathalani shirika hilo liliweza kupata na kusambaza huduma hizo pamoja na nyingine za afya ya uzazi licha ya gharama kubwa zilizoongezeka za vifaa hivyo.

Mathalani kutumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu za kiganjani, kutoa huduma za ushauri nasaha kwenye vituo vya karantini vya COVID-19.