Kinachotokea Yemeni ni aibu kwa ubinadamu - WFP

11 Machi 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani wa Umoja wa Mataifa, WFP, David Beasley akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Yemen, ametoa ombi la dharura la amani nchini humo na akatoa wito wa ufadhili ili kusaidia familia zilizo na hali ya hatari zaidi kutokana na njaa kali zaidi kuwahi kushuhudiwa na ulimwengu katika zama za sasa.  

Katika hospitali ya Al Sabeen mjini Sana’a, Mkuu hyo wa WFP Bwana Beasley alikutana na Sultan, mtoto wa umri wa miaka 2 anayetibiwa utapiamlo kwa ufadhili wa WFP. Nusu ya watoto wote chini ya miaka mitano nchini Yemen, yaani watoto milioni 2.3 wanakadiriwa kukabiliwa na utapiamlo mkali mwaka huu, na karibu watoto 400,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wanaweza kufariki dunia ikiwa hawatapata matibabu ya haraka. 

Baada ya kuwatembelea watoto wenye utapiamlo, Bwana Beasley anasema,  “baada ya miaka 6 ya vita na kuzorota sana kwa uchumi, ukosefu wa pesa, ukosefu wa rasilimali. Nimesimama hapa katika chumba hiki cha hospitali ambapo mtoto huyu, haswa yuko katika hatihati ya kufa, kwa sababu hawana chakula, hawana vifaa vya matibabu na vinginevyo vya kuwatunza. Na kwa hivyo, tuna mamilioni ya watoto ambao maisha yao yako hatarini kwa kweli watoto 400,000 wako katika hatari ya kufa hivi sasa. Tunahitaji vita hii kumalizika na tunahitaji msaada kifedha, chakula, lishe, vifaa vya matibabu na tunavihitaji sasa. Ni hali ya kutisha. Ni aibu kwa ubinadamu kile kinachotokea hapa.” 

Mwananchi huyu wa Yemen akiandaa mlo kwenye kambi isiyo rasmi ya wakimbizi wa ndani ya Dar Saad mjini Aden nchini Yemen.
UN OCHA/GILES CLARKE
Mwananchi huyu wa Yemen akiandaa mlo kwenye kambi isiyo rasmi ya wakimbizi wa ndani ya Dar Saad mjini Aden nchini Yemen.

Beasley pia aliona maendeleo ya mpango wa usajili wa kielekroniki wa WFP, akihakikisha msaada wa chakula unatolewa kwa uwajibikaji na uwazi. 

WFP inaangalia njia zote ili kuongeza msaada ili kukidhi mahitaji ya kuongezeka na kuzuia njaa inayotisha na tayari inatoa kipaumbele kwa msaada wa kila mwezi kwa wilaya 11 zenye watu katika hali inayoelekea kuwa ya njaa na kwa lengo la kuokoa maisha na kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.  

WFP inasema Meli kumi na nne zilizobeba mafuta kwa sasa zinashikiliwa katika pwani ya Bahari ya Shamu ukanda wa Yemen na haziwezi kutia nanga. Pamoja na akiba ya mafuta kukaribia kuisha, hospitali zimeachwa bila umeme na sekta ya kibiashara ikijitahidi kusafirisha chakula na bidhaa za kimsingi. Hakuna meli ambayo imemudu kuingia katika bandari ya Al Hodeidah tangu tarehe 3 Januari mwaka huu 2021. 

Operesheni ya WFP inabaki ikiwa na ufadhili mdogo sana na uwezo wa shirika kudumisha kiwango hiki cha huduma uko hatarini.  WFP inahitaji dola za kimarekani bilioni 1.9 bilioni ili kuokoa maisha na kutoa msaada wa chakula katika mwaka huu wa 2021. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter