Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda inahitaji kupigwa jeki iweze kuendelea kukirimu wakimbizi:Grandi

Mkimbizi Cavine Abalo mwenye umri wa miaka 20 akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi mitatu katika wilaya ya Lamwo nchini Uganda.
UNICEF/Jimmy Adriko
Mkimbizi Cavine Abalo mwenye umri wa miaka 20 akiwa na mwanae mwenye umri wa miezi mitatu katika wilaya ya Lamwo nchini Uganda.

Uganda inahitaji kupigwa jeki iweze kuendelea kukirimu wakimbizi:Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi akiwa ziarani nchini Uganda amesema taifa hilo linastahili na linahitaji kupigwa jeki ili liweze kumudu changamoto za wakimbizi linaowahifadhi na kuendelea kukirimu wengine.

Katika makazi makubwa kabisa ya wakimbizi barani Afrika ya Bidibbidi Uganda, Kamishina Grandi akizuru kituo cha maji kinachoendeshwa na mitambo ya sola kama sehemu ya ziara yake nchini humu. 

Bidibidi inahifadhi wakimbizi zaidi ya 235,000 kutoka Sudan Kusini na mtambo huu wa maji unatoa huduma kwa zaidi ya watu 18,000 wakimbizi na jamii za wenyeji. 

Baada ya kupatiwa maelezo  kuhusu kituo hiki alielekea kwenye shule ya msingi ya Twajiji ambako amepata fursa ya kujionea vyumba vipya vya madarasa vilivyojengwa kwa hisani ya benki ya maendeleo ya Ujerumani ambayo pia inasaidia kulipa mishahara ya waalimu na kuendesha shule hiyo. 

Hapa amezungumza na waalimu na wanafunzi na kusikia changamoto zao. 

Grandi pia ametembelea mradi wa ujenzi wa nyuma za wakimbizi zinazojengwa na wakimbizi wenye wakishirikiana na wenyeji na kuzungumza na Agnes Batio mkimbizi kutoka Sudan Kusini anayesimamia mradi huo ambao unaotoa mafunzo ya ujenzi pia kwa wakimbizi na wenyeji.

Grandi alitaka kufahamu kilichomsukuma Agnes kujiunga katika ujenzi na Agnes akasema, “nilipendelea ujenzi kwa sababu nilipokuwa Sudan Kusini, nilimuona mwanamke akishiriki kazi ya kujenga, nami nikaipenda na pia ninataka kuwa kama yeye. Najua wanawake wana uwezo wa kufanya chochote ndio sababu nimeingia kwenye kazi hii kwa kuwa hakuna wanawake wengi ambao wanaifanya.” 

Baada ya kutembelea miradi na shughuli zingine kamishina mkuu akakutana na wanawake ambao wanawakilisha jamii yao ya wakimbizi kwenye jukwaa la kitaifa la ushiriki wa wakimbizi lililoanzishwa mwaka 2018 ili kuhakikisha sauti zao, hofu zao na matatizo yao yanawasilishwa. 

Grandi amekiri kwamba kuna changamoto kubwa Uganda na amelishukuru taifa hilo kwa ukarimu wake akisema,  "Uganda imedhihirisha ukarimu wa hali ya juu na wa aina yake ikiwemo wakati huu mgumu wa COVID-19 ambapo watu kutembea inakuwa ni hatari sana, lakini bado ukarimu wake umeendelea, japo maisha yameathirika kwa sababu ya kushindwa kutioka sehemu moja hadi nyingine na uhaba wa shughuli za kiuchumi, hivyo msaada zaidi unahitajika kwa upande huo.” 

Uganda inahifadhi wakimbizi milioni 1.45 na asilimia kubwa ni kutoka Sudan Kusini ikifuatiwa na DRC.