Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumalizika mgawanyiko wa kimataifa kuhusu Syria ni jawabu kwa mzozo wa Syria- Guterres

Dkt. Akjeman Magtgmova, Mwakilishi wa WHO nchini Syria akiwa amembeba mtoto kwenye moja ya kituo cha afya nchini humo.
WHO Syria
Dkt. Akjeman Magtgmova, Mwakilishi wa WHO nchini Syria akiwa amembeba mtoto kwenye moja ya kituo cha afya nchini humo.

Kumalizika mgawanyiko wa kimataifa kuhusu Syria ni jawabu kwa mzozo wa Syria- Guterres

Amani na Usalama

Baada ya muongo mmoja wa mapigano nchini Syria, bado taifa hilo limesalia matatizoni tena katikati ya janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hii leo akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani wakati mzozo wa Syria ukitimu miaka 10.

Katibu Mkuu amesema, “miaka 10 iliyopita, ghasia dhidi ya maandamano yakupinga ukandamizaji nchini Syria zilitumbukiza taifa hilo katika vita vya kutisha. Sasa Syria imesahaulika na bado maisha ya wasyria ni kama jinamizi.”

Hali ya machungu

ya maelfu ya wasyria wameuawa. Mamilioni wamekimbia makazi yao, idadi isiyohesabika wanashikiliwa kinyume cha sheria, wanateswa, wametoweshwa au wanaishi katika maisha dhalili.

Guterres amesema kwa miaka 10, dunia imeshuhudia Syria ikitumbukia kwenye uharibifu na umwagaji damu huku wananchi wakitumbukia katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kiasi kikubwa na kwa mfumo wa aina yake.

Tarehe 19 Januari mwaka 2021,watoto wakiwa nje ya mahema yaliyozingirwa na maji kwenye kambi ya Kafr Losin Kaskazini-Magharibi mwa Syria.
© UNICEF/Khaled Akacha
Tarehe 19 Januari mwaka 2021,watoto wakiwa nje ya mahema yaliyozingirwa na maji kwenye kambi ya Kafr Losin Kaskazini-Magharibi mwa Syria.

Pande kinzani katika mzozo huo nazo mara kwa mara zimeendelea kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na bila kukumbwa na mkono wowote wa sheria. “Mabomu na makombora yamemiminikia nyumba, shule, hospitali na masoko. Silaha za kikemikali zimesababisha machungu ya kupitiliza. Miji imeweka vizuizi na vikwazo dhidi ya misaada ya kibinadamu, miji mingine imezingirwa hivyo raia kusalia na njaa,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu amesema ni vigumu kupata taswira halisi ya uharibifu nchini Syria, lakini wananchi wake wamepitia uhalifu mkubwa zaidi dunia kuwahi kushuhudia karne ya sasa.

Amesema hakuna familia iliyokuwa salama, takribani nusu ya watoto hawajamaliza siku bila vita akiongeza kuwa, “machungu yanazidishwa na kuporomoka kwa uchumi, ongezeko la umaskini uliosababishwa na mapigano, ufisadi, vikwazo na janga la COVID-19.”

Mhudumu wa afya akizungumza na watoto wakimbizi kuhusu matumaini na hofu zao kwenye kambi ya Atma nchini Syria.
© UNOCHA/Mahmoud Al-Basha
Mhudumu wa afya akizungumza na watoto wakimbizi kuhusu matumaini na hofu zao kwenye kambi ya Atma nchini Syria.

Msaada wa kibinadamu bado muhimu

Njaa nayo yanyemelea asilimia 60 ya wananchi wa Syria mwaka huu ambapo amesema Katibu Mkuu ni vyema kuendelea kuwafikishia msaada wa kibinadamu wahitaji nchini humo.

“Msaada zaidi wa kibinadamu unahitajika nchini Syria. Usambazaji na usafirishaji wa misaada kuvuka mipaka na maeneo ya mizozo ni muhimu ili kufikia kila mtu na kila pahali,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza kuwa ndio maana mara kwa mara amelisihi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufikia maridhiano kuhusu suala hilo muhimu.

Suluhu ya kisiasa ni muarobaini

Bwana Guterres amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaka suluhu ya kisiasa nchini Syria kwa mujibu wa azimio namba 2254 la Baraza hilo la Usalama, akisema hatua ya kwanza muhimu kuelekea mwelekeo huo ni maendeleo thabiti kwenye kamati ya kikatiba.

Amesisitiza kuwa pande husika nchini Syria zina fursa ya kuonesha utayari wa kusaka msimamo mmoja na kutambua umuhimu wa wasyria wote ambao wanawawakilisha wanasonga mbele na kuondokana na hali ya mapigano.

Guterres amesema ni mchakato ambao wanawake na wanaume wa Syria wanapaswa kushiriki kikamilifu na ambao hatimaye jamii nzima ya wasyria watashiriki.

Hata hivyo amesema itahitaji kuondoa tofauti iliyopo kwenye jamii ya kimataifa kupitia mashauriano endelevu na ya dhati ya kidiplomasia huku akisisitiza kuwa, “kinyume cha hapo ni saw ana kuendelea kuwatumbukiza wasyria katika kukata tamaa, jambo ambalo hatuwezi kukubali litokee.”