Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujenga barabara, kunajenga amani kupitia kuunganisha jamii - UNMISS 

Walinda amani wa UNMISS wakiwa katika ulinzi Sudan Kusini. (Maktaba)
UNMISS
Walinda amani wa UNMISS wakiwa katika ulinzi Sudan Kusini. (Maktaba)

Kujenga barabara, kunajenga amani kupitia kuunganisha jamii - UNMISS 

Amani na Usalama

Wahandisi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS kutoka nchi saba tofauti wanatumia fursa ya msimu wa kiangazi unaoendelea kukarabati kilomita 3,200 za barabara nchini Sudan Kusini. Wahandisi kutoka Bangladesh wamekishika kipande kinachounganisha Rokon na mji Mkuu Juba. 

Shughuli za kuchimba na kuhamisha udongo zinaendelea katika eneo la Jambo nchini Sudan Kusini. Katika Jimbo la Equatoria ya kati, wahandisi wa Bangladesh wanaouhudumu katika UNMISS wameweka viraka katika kilomita 130 za barabara inayounganisha Rokon na mji Mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Meja Raihan ni mhandisi kutoka Bangladesh anasema, “tumekuja hapa tarehe 14 Januari kuanza mradi wa ukarabati wa barabara. Hadi sasa, tumekarabati kilomita 130 ambayo ni asilimia 45 ya mradi wote. Tumebakiwa na kilometa 170 ambazo tutazimaliza katika siku zinazofuata.” 

Kazi inaenda polepole na inachosha kwa kuwa eneo hili lina joto kali na fukuto. Hata hvyo walinda amani hawa wamefanya maendeleo makubwa ya kushangaza. Luteni Jenerali Shailesh Tinaikar ni Kamanda wa Kikosi, UNMISS anasema, “kazi yao inathaminiwa na kila mtu. Inaunganisha jamii, inaruhusu watu kusafirisha bidhaa, imepunguza umbali kati ya Rokon na Juba. Nilikuwa nikiongea na wasimamizi wengine wa kaunti hapa na muda ambao unatumia pindi ambapo barabara zinakuwa katika hali mbaya ni saa nane hadi kumi. Leo, kwa matengenezo yanayofanywa na wahandisi wa Bangladesh, muda umepunguzwa hadi saa mbili." 

Wanajamii nao wanathamini juhudi za UNMISS za kuboresha miundombinu ya barabara, kuwawezesha kukusanyika na kuungana. Noel Ladu ni Naibu Mkurugenzi wa uongozi wa eneo hilo anasema,“matengenezo ya barabara hii ni muhimu sana kwetu kwa ajili ya uchumi kijamii kwetu sisi sote hapa. Ukiangalia barabara hii kama ilivyokuwa awali, watu hawakuweza kufika Juba. Lakini UNMISS imefanya kazi nzuri sana; ukiangalia magari yanatembea polepole na vizuri kuelekea Juba.” 

Katika nchi hii iliyo na kilomita 400 tu za barabara za lami, kuboresha barabara kunaongeza  mawasiliano, biashara, ajira, na muhimu zaidi, kunajenga amani kupitia kuunganisha jamii. 

TAGS: UNMISS, Sudan Kusini, Bangladesh